SIMBA YATINGA FAINALI YA FA, YAICHAPA AZAM 1-0 … yanusa michuano ya kimataifa


Simba imefanikiwa kutinga fainali ya Azam Sports Federation Cup baada ya kuifunga Azam FC 1-0 kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikosi cha Simba sasa kitacheza na mshindi wa nusu fainali itakayopigwa kesho jijini Mwanza kati ya Yanga na Mbao FC ya Mwanza.

Bao pekee la Simba lilifungwa na Mohamed “Mo” Ibrahim kunako dakika ya 48 akimalizia krosi safi ya Mavugo.

Iwapo Yanga itaitoa Mbao FC, basi Simba itakuwa imepata tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao bila kujali nani atakuwa bingwa.

Tiketi hiyo inakuja kutokana na ukweli kuwa kimahesabu Simba na Yanga ndizo zitakazomaliza kwenye nafasi mbili za juu za Ligi Kuu ya Vodacom.

Iwapo Yanga itatwaa Ligi Kuu ubingwa wa Vodacom na FA (Azam Sports Federation Cup), basi nafasi ya pili ya kushiriki michuano ya kimataifa itakwenda kwa Simba.

Azam ilicheza pungufu tangu dakika ya 16 baada ya kiungo Salum Abubakary “Sure Boy” kulambwa kadi nyekundu, huku mshambuliaji Mohamed Ibrahim wa Simba naye akitolewa dakika ya 77 baada ya kupewa kadi ya pili ya njano.

No comments