TAMBWE ASIFU BAO LA MKONO ALILOWAFUNGA SIMBA KIMAGUMASHI

MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, Amisi Tambwe raia wa Burundi ametonesha kidonda cha Simba baada ya kusema kuwa bao alilowafunga kwa mkono ndio goli lake bora tangu atue kucheza Ligi Kuu Bara.

Mshambuliaji huyo alisema kwamba amekuwa akifunga mabao mengi mazuri kila msimu lakini lile alilowafunga Simba lilikuwa bora zaidi katika maisha yake ya soka.

“Yapo mabao mengi tu nimefunga na mazuri, nakumbuka hata Mbeya City niliwafunga bao zuri ila niweke wazi kuwa lile nililowafunga Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ndio bao bora zaidi katika maisha yangu ya soka,” alisema Tambwe ambaye bao lake lilikuwa gumzo akilaumiwa kuunawa mkono kabla ya kufunga.

“Nilifunga katika mazingira magumu mbele ya mabeki wawili wa Simba, haijalishi kama niliunawa kabla au la lakini kwangu ndio bao bora,” aliongeza mkali huyo wa mabao.

Bao alilofunga Tambwe lilikuwa ni kwenye mechi ya awali dhidi ya watani katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania bara ambapo mchezo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 huku Simba ikisawazisha kupitia Shiza Kichuya aliyefunga kwa njia ya kona.


Amisi Tambwe alipotua nchini msimu wake wa kwanza alifanikiwa kuwa mfungaji bora akiwa kwenye kikosi cha Simba kabla ya kutua Yanga ambapo pia aliibuka mfungaji bora wa Ligi.

No comments