TFF YA JAMALI MALINZI KUBURUZWA MAHAKAMANI NA WANAZI WA SOKA LA BONGO

WINGU jeusi linaweza kuharibu kabisa taswira ya soka Tanzania kuanzia wiki ijayo, saluti5 imeambiwa.

Habari ambazo mtandao huu umezipata jana zinasema kwamba wadau watatu ambao ni wapenzi wa kawaida kabisa wa michezo, wako katika hatua za mwisho za kulifungulia kesi Shirikisho la mpira wa miguu hapa nchini (TFF).

Pamoja na wengine watatu hao ambao wanadaiwa kuungwa mkono na mashabiki wengi, wanataka kuiomba mahakama kutoa amri ya kusimamisha Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara hadi hapo utakapopatikana ufafanuzi wa tafsiri ya mchezaji mwenye kadi tatu za njano kucheza mechi zinazofuata.

Wadau hao ambao majina yao yanaifadhiwa kwa sasa kutokana na sababu za kiusalama, wanadaiwa kutumia kielelezo cha sakata la mchezaji Mohammed Fhaki wa Kagera Sugar ambaye Simba ilimkatia rufaa na ikapewa pointi tatu ambazo ilizipoteza uwanjani walipocheza na Kagera mjini Bukoba mwanzoni mwa mwezi huu.

Kamati ya masaa 72 ya TFF iliamua kuipa Simba pointi tatu na mabao matatu baada ya kuridhika kuwa Fhaki alikuwa na kadi tatu za njano kabla ya mechi ya Simba.

Lakini Kagera Sugar walilalamika na kuomba kurejewa kwa maamuzi hayo na Kamati ya Sheria, Haki na Hadhi ya Wachezaji katika kikao chake ikarejeshea Kagera pointi hizo tatu.

Jambo hilo limewatia simanzi mashabiki wengi wa soka hapa nchini na wameonekana kuondokwa na imani ya TFF inayoongozwa na rais wake Jamal Malanzi.

“Watu wameamua kusaka tafsiri ya sheria mahakamani ingawa tunajua baada ya kufunguliwa kwa kesi hiyo mambo yote ya mpira yatakuwa yamesimama,” amesema mmoja wawatoa habari hizo.

“Wakili aliyepewa kazi hiyo ameshaandika hati ya maombi ngoja tuone nini kitatokea,” amesema.


Kama kesi hiyo itafunguliwa inaweza kuhathiri kabisa Ligi Kuu inayokaribia kumalizika, lakini pia inaweza kuifanya timu ya taifa chini ya miaka 17 inayoshiriki Kombe la Mataifa Afrika nchini Gabon kuondolewa kwenye mashindano hayo.

No comments