THIERRY HENRY ATOA LA ROHONI KWA WENGER, ASEMA WACHEZAJI MASHUHURI WANAIKACHA ARSENAL


Thierry Henry amesema klabu yake ya zamani, Arsenal iko nyuma ya wapinzani wake wakubwa linapokuja suala la usajili wa wachezaji.

Katika makala yake kupitia gazeti za The Sun la Uingereza, Thierry akaandika kuwa Arsenal imepoteza mvuto kwa wachezaji mashuhuri.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal akasema timu hiyo ilishindwa kumyakua N’Golo Kante  kutoka Leicester  na kujiunga na Chelsea, Zlatan Ibrahimovic akatua Manchester United.

"Kante alikuwa 'lulu' kwenye usajili wa kiangazi na akachagua Chelsea badala ya Arsenal ambayo nayo ilimtaka," anandika Thierry.

"Arsenal ilimaliza ya pili kwenye Premier League msimu uliopita, Chelsea ilimaliza katikati ya msimamo lakini bado kiungo  huyo wa Leicester akachagua Chelsea - na sasa hajutii uamuzi wake. Wanaelekea kuchukua taji moja au zaidi," anaendelea kuandika Thierry.

Thierry anasema wachezaji wote mashuhuri wanataka kucheza Champions League  - lakini Kante akabaini kuwa msimu huo mmoja hauwezi kuharibu njozi zake.

"Ni ngumu kulinganisha, lakini wakati nachezea Arsenal kulikuwa na wachezaji wengi wakubwa wanataka kujiunga na timu yetu, tungeweza kuchuana  kiuchumi, pengine si  na Manchester United lakini kwa timu zote zilizobakia tuliweza kushindana nazo.

"Lakini sasa pesa zinamwagiga kutokana na malipo ya haki za TV, vilabu vingi vinaweza kuchuana kwenye usajili. Kwahiyo unatakiwa kuwa na mvuto na matarajio makubwa ili klabu yako iweze kuvutia wachezaji wenye vipaji," anaeleza Henry.

Mshambuliaji huyo anataja mshahara kama moja ya vivutio kwa vile mpira ni kazi kama kazi nyingine na hivyo mwisho wa siku kila mchezaji lazima aangalie maslahi yake.

Lakini Thierry anasema uwezo wa klabu kutwaa mataji, ni sababu kubwa zaidi. "Kama wewe ni mkurugezi wa soka na unafanya kazi Arsenal, ni namna gani unaweza kushawishi wachezaji wakubwa?" anahoji Thierry Henry.


"Sisemi kuwa watu hawatimizi wajibu wao Arsenal - lakini najaribu kuonyesha kuwa kuinadi klabu hii imekuwa jambo gumu kwa miaka miwili au mitatu iliyopita. Sioni kivutio chochote kwa wachezaji wakubwa".

No comments