VIJEMBE VYA KHADIJA YUSSUF, FATMA MCHARUKO VYATAWALA PAMBANO LA "NANI ZAIDI"

WAKATI pambano linalowakutanisha mastaa watano wa taarab TZ linatazamiwa kufanyika kesho Jumapili, lakini upinzani mkubwa zaidi unaonekana kuwa kati ya Fatma Mahmoud “Mcharuko” na Khadija Yussuf “Sauti ya Chiriku”.

Wasanii wengine watatu waliomo kwenye pambano hilo lililopewa jina la “Nani Zaidi”, ni Mwasiti Kitoronto, Hanifa Maulid na Mwamvita Shaibu.

Kupitia sauti za msanii mmoja mmoja kwenye matangazo yao, Fatma na Khadija wameonekana kutupiana vijembe vya chini kwa chini ambavyo kwa mashabiki na wadau wengi vimejenga picha ya kuwa “wanatafutana”.

Mara kadhaa, Mcharuko amekuwa akijinadi kwamba atatinga kwenye pambano hilo kifua mbele bila kuwahofia waliopania “kufungia mbwa bandani”, akimaanisha Khadija Yussuf na Wakaliwao Modern Taradance ambao hiyo ndio kaulimbiu yao kubwa.

Nae Khadija amekaririwa mara kwa mara akirudisha majibu kwa kusema ya kuwa yeye ndie nyakanga wa wasanii wote wanaoshiriki pambano hilo na kwamba “anawajua” fika lakini “wao” hawajui alipoanzia.

Inawezekana kuwa kweli wasanii wengine wote kwqenye pambano hilo hawajui alipoanzia Khadija, lakini kwa upande wake Khadija anayeweza kumjua “fika” kimuziki ni Mcharuko pekee aliyewahi kuwa nae bendi moja ya Jahazi Modern Taarab.

Hali hiyo ya vijembe vya chini kwa chini imefanya mashabiki wengi kuhisi kuwa wawili hao wanakamiana, huku wengine wakifika mbali zaidi kwa kubashiri kuwa kazi itakuwepo pale kila mmoja atakapotaka kumuonyesha mwenzake jukwaani.

No comments