WACHEZA JUDO WAZIDI KUJIWEKA SAWA NA MASHINDANO YA DUNIA AGOSTI, MWAKA HUU

CHAMA cha Judo Tanzania (JATA), kimesema kwamba wachezaji wa timu ya taifa wa mchezo huo wa Judo wanaendelea kujiandaa kwa ajili ya mashindano ya dunia yatakayofanyika mwezi Agosti, mwaka huu.

Akiongea na saluti5 Katibu mkuu wa JATA, Innocent Maly alisema kuwa sanjali na maandalizi hayo, wachezaji hao wana fursa ya kwenda kambi ya kimataifa kwa ajili ya Olimpiki 2020 itakayofanyika nchini Hungary.

Alisema kuwa wachezaji watatu akiwemo Mussa Sheki (kg 100), Andrew Thomas (kg 73) na Omary Uledi (kg 66), wakiwa chini ya kocha Omary Mgole, wako kambini kwa maandalizi hayo.

Maly alisema kuwa kwa sasa chama kipo katika mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya maandalizi ya wachezaji hao.
“Wachezaji hao wote wanaendelea na maandalizi tukiwa pia tunatafuta fedha na zitakapopatikana ndio tutajua tutawapeleka wangapi kwa mujibu wa mfuko wetu,” alisema Maly.

Katibu huyo alisema kuwa malengo ya chama ni kuhakikisha wanatumia fursa ya kuwapeleka wachezaji kwa ajili ya kambi ili kujipanga kwa mashindano ya kimataifa.


Ametoa wito kwa wadau nchini kujitokeza kusapoti mchezo huo ili kupata fedha kwa ajili ya timu ya Taifa iweze kwenda kufanya vizuri kimataifa.

No comments