WACHEZAJI YANGA SASA WAAMUA KUPOTEZEA CHANGAMOTO ZA MASLAHI YAO NA KUUNGANA "KUKOMALIA" UBINGWA

WAKIWA kwenye maandalizi ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mbao FC ya jijini Mwanza, wachezaji wa Yanga wametoa tamko kuwa ni wakati wa kuweka chini matatizo yao na kupigania klabu katika kipindi hiki cha mpito.

Wachezaji pamoja na wanachama kwa nyakati tofauti wamezungumza na saluti5 na kusema kwamba wamelazimika kusahau changamoto zilizopo ili kuhakikisha azma yao ya kutetea makombe yote ambayo walitwaa msimu uliopita, inatimia.

Nahodha wa kikosi cha Yanga, Nadir haroub “Cannavaro” alisema kuwa wamepania kulinda heshima ya klabu kwa kutwaa makombe yote yaliyoko mbele yao.

“Hatuna muda wa kutazama changamoto zinazoelezwa na vyombo vya habari dhidi yetu, kila kitu tumekiacha kwenye mikono ya uongozi, sisi kazi yetu ni kuhakikisha tunatetea makombe yote mawili kwa hali yoyote ile,” alisema beki huyo mkongwe zaidi kwenye kikosi cha Yanga.

“Kama timu tumeamua kuungana na kupigania hadhi ya klabu yetu kwa kubeba makombe yote, nadhani hiyo itakuwa njia sahihi ya kurejesha heshima yetu,” aliongeza Cannavaro.

Yanga inaingia kwenye mchezo dhidi ya Mbao FC ikiwa na hali ya kujiamini baada ya kuifunga Tanzania Prisons kwa mabao 3-0 katika mchezo war obo fainali.

No comments