‘WEEKEND BONANZA’ YAWAPA ZA USO MARAPA WA DANSI WALIOKIMBILIA SINGELI


Marapa wa muziki wa dansi waliojitosa kwenye muziki wa singeli wamefananishwa na watu waliofilisika mawazo.

Hayo yalisemwa jana usiku kupitia kipindi cha Weekend Bonanza cha Clouds FM ambapo marapa hao walitajwa kuwa wameishiwa mbinu za kuukwamua muziki wa dansi na sasa wamekimbilia kutoa nyimbo za singeli.

Mtangazaji na mwendeshaji wa kipindi hicho Khamis Dacota (pichani juu) sambamba na dj wa kipindi hicho cha Weekend Bonanza, Dj Bullah, walitaja hatua hiyo kama anguko la kisanii.

Weekend Bonanza huruka kila Jumamosi kuanzia 4 usiku hadi saa 7 usiku na hupiga muziki wa kiafrika huku dansi likipewa kipaumbele cha hali ya juu.

“Hawa marapa wa dansi waliokimbilia kutoa nyimbo za singeli wamefeli. Katika mapambano huwezi kumsubiri adui yako aingie hadi ndani eti indo umpige vizuri. Hebu wajifunze kwa Bill Clinton aliyekuwa kwa Werrason, ni mkongwe lakini mpaka leo hajaacha njia zake na bado anatamba kwa vibao vikali,” alisema Dj Bullah.

“Marapa waliokimbilia singeli wanashangaza sana, muziki wao dansi umeyumba hawana vionjo na sasa wanalikimbia eneo lao, hii ni dhahiri kuwa hawana ubunifu,” alisema Dacota.

 “Kama wameshindwa kusimamia ama kupambana kurudisha hadhi yao na ubora wa rap zao na badala yake wamekimbilia kwenye singeli huku ni kufeli. Wanakwenda kutafuta kura za huruma kwa  kuwabana vijana wa watu ambao wanapambana kusaka mafanikio kupitia muziki wao wa singeli,” aliongeza Dacota.

Ingawa Weekend Bonanza haikutaja majina ya marapa au waimbaji wa dansi waliohamishia nguvu kwenye singeli, lakini Saluti5 inafahamu ushiriki wa Khalid Chokoraa, Kalala Jr, Kitokololo, Papy Catalogue na Mirinda Nyeusi katika muziki wa singeli kwa siku za hivi karibuni.

No comments