YANGA "ILIYOFULIA" YAONYESHA JEURI YA FEDHA, YAKODI NDEGE KUIFUATA MBAO FC MWANZA

PAMOJA na taarifa zilizoenea mtaani kuwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamefulia, bado uongozi wa klabu hiyo umeonyesha kumudu baadhi ya masuala muhimu, ikiwemo kukodi usafiri wa anga kwa ajili ya kuwafuata Mbao FC kibabe jijini Mwanza.

Kufuatia umuhimu wa mchezo huo na nia ya Yanga kutetea ubingwa wa Kombe la FA, uongozi wa klabu umeamua kukodi ndege ili kurahisisha safari hiyo na kuwaondolea uchovu nyota wake kabla ya mchezo.

Yanga itamenyana na Mbao FC kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA siku ya Jumapili katika uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Mabingwa hao watetezi wa michuano ya FA walitinga hatua hiyo baada ya kuifunga timu ya Prisons ya Mbeya kwa mabao 3-0 katika mchezo uliochezwa jijini Dar es Salaam.

Baada ya mchezo huo kumalizika, klabu hiyo itasalia mkoani Mwanza kwa ajili ya kambi ya muda mfupi kujiandaa na mchezo wake dhidi ya Prisons utakaopigwa Mei 6, katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.


Hiyo itakuwa moja kati ya mechi za viporo ambavyop Yanga ilivikosa wakati inawakilisha Taifa kwenye michuano ya Kombe la CAF.

No comments