AISHI MANULA, KAPOMBE KUUNGANA NA JOHN BOCCO ANAYETARAJIWA KUTUA SIMBA

SASA ni dhahiri kwamba aliyekuwa nahodha wa Azam FC, John Bocco “Adebayor” ni mali ya wekundu wa Msimbazi, klabu ya Simba.

Azam juzi ilisema kwamba imemalizana na nahodha wake huyo na hatakuwa sehemu ya kikosi chake kipya cha msimu wa 2017/18.

Ofisa habari wa Azam, Jafar Idd maganga aliwaambia waandishi wa habari kwamba Bocco ni mchezaji huru na anaweza kwenda kokote.

Lakini habari zinasema kwamba nyota huyo ameshaingia makubaliano na Simba na kusaini mkataba wa miaka miwili.

Wakati hilo likiwa sio siri tena, habari zinasema kwamba Bocco amewavutia wanasoka wengine wawili wa klabu hiyo ya Chamazi, kipa namba moja Aishi Manula na beki wa kulia, Shomari Kapombe kujiunga Simba.

Ingawaje katika akaunti yake Manula amekanusha kwamba bado hajasaini Simba, lakini fununu zinasema kwamba kipa huyo ni kama ameshatanguliza mguu mmoja Simba.

Maganga mwenyewe amesema wachezaji hao bado wana mkataba na Azam wa mwezi mmoja zaidi na hakutaka kuzungumzia zaidi uhamisho wao unaovuma sasa kwamba wanakwenda Simba.

Simba pia wanataka kumrejesha Kapombe katika kikosi hicho ambacho amekitumikia kwa mafanikio makubwa zaidi.

Kapombe alikuwa kiraka katika Simba na baadae akauzwa kwenye klabu ya AS Cannes ya Ufaransa lakini baadae akavunja mkataba na kujiunga na azam FC ya hapa nchini. 

“Kimsingi unaona wazi kwamba Azam kuna matatizo kidogo. Kuna baadhi ya wachezaji haswa wazawa wanaona kwamba klabu haina mwelekeo na tangu kuondoka na baadae kufariki kwa aliyekuwa mwenyekiti wake mzee Said Mohammed, kuna kitu kinakosekana Azam,” chanzo chetu kimesema.

Kapombe na Manula wanadaiwa kuwa wao wenyewe wanashawishika kumfuata nahodha wao, Bocco katika klabu ya Simba.

Manula amesema katika akaunti yake ya Instagram kwamba bado angependa kubaki katika klabu iliyomlea ya Azam.

Kapombe hakupatikana kuzungumzia jambo hilo na saluti5 ilipomtafuta simu yake ilikuwa haipatikani.

No comments