AYA 15 ZA SAID MDOE: AHSANTENI MSONDO NA SIKINDE KWA DARASA MUJARAB, EL CLASICO MJIPANGE UPYA


Wikiendi iliyopita yalifanyika maonyesho mawili makubwa ya muziki wa dansi ndani ya kumbi za Escape One Mikocheni na Travertine Hotel Magomeni ambapo msisimko uliokuwepo kuelekea maonyesho haya, ulikuwa wa hali ya juu.

Wakati Ijumaa pale Escape One lilikuwepo onyesho la mpambano wa magwiji wa tatu – Ally Chocky, Mwinjuma Muumin na Nyoshi el Saadat, Travertine ilikuwa ni ‘mechi’ kali ya Msongo Ngoma na Sikinde Ngoma ya Ukae siku ya Jumamosi.

Kwa bahati mbaya sana, maonyesho yote mawili hayakumalizika, yalivunjika baada ya kushuka mvua kubwa, moja likivunjika saa 8 usiku na lingine saa 6 usiku.

Pamoja na kuvunjika kwa maonyesho hayo, lakini kuna mengi ya kujifunza kwaajili ya usatawi wa matukio makubwa ya kiburudani kama haya kwa siku zijazo. Kuna sehemu zinahitaji kupongenzwa na zipo sehemu zinazostahili lawama.

Waratibu wa Msondo na Sikinde waliuetendea haki muda, walijua kuisimamia ratiba, walikuwa na weledi wa kuwapa mashabiki kile walichokifuata pale – Msondo na Sikinde, si kingine. Kiingilio cha sh. 10,000 nacho kilikuwa sahihi kulingana na hali ya uchumi ilivyo hivi sasa.

Mahudhurio makubwa ya Mashabiki yaliyojitokeza Travertine, ni ushihidi kuwa mambo yakipangiliwa kisayansi, muziki wa dansi bado una soko kubwa.

Saa 3 kamili show ilianza na kila bendi ilipangiwa kutumbuiza kwa saa moja ambapo ratiba ingeendelea hivyo hadi mwisho wa onyesho. Ilikuwa ni juu ya bendi kuamua namna ya kutumia dakika 60 ilizopangiwa – kama itapiga nyimbo mbili, tatu au nne hiyo ni juu yao ili mradi isivuke muda uliopangwa.

Hadi mvua inanyesha saa 6 usiku, Sikinde walishapiga raundi mbili na Msondo raundi moja. Ilikuwa ni nidhamu ya hali ya juu katika uzingatiaji ratiba na muda.

Laiti kama onyesho lile lingekuwa na blah blah nyingi pamoja na show za wasindikizaji, ikiwemo ule ‘uswahili’ wa kuchelewa kuanza show ili wateja wajae, basi pengine mvua ile ingevunja show kabla hatujaiona Sikinde wala Msondo.

Na hapo ndipo unapopata tofauti ya kwanza ya show ya Msondo na Sikinde dhidi ya ile ya kina Chocky, Muumin na Nyoshi iliyopewa jina la El Clasico.


Show ya El Clasico mtumbuizaji wa kwanza alikuwa Muumin kunako saa 6:23 usiku ambapo alitumbuiza hadi saa 7:35. Kwa ratiba hiyo pata picha iwapo show hii ndiyo ingekumbwa na mvua saa 6 kamili za usiku ingekuweje!

Kama vile hiyo haitoshi, baada ya Muumin kushuka, waandaji ambao hawakuweka wazi mpangilio wa kutumbuiza kwa magwiji hao ukoje, wakathubutu kuwapandisha wasindikizaji wengine saa 7:40, wakala muda hadi saa 8 na kilichofuata baada ya hapo ni mvua kubwa iliyovunja show kabla Nyoshi na Chocky hawajatumbuiza.

Kwa kifupi show ya El Clasico ilifeli kwa mengi – mahudhurio hafifu, ratiba mbovu, kiingilio kikubwa (15,000) na utitiri wa wasindikizaji ambao hata wao walichelewa kupandisha jukwaani. Mtumbuizaji wa kwanza MC Soudy alipandishwa saa 5.30 na iwapo Khadija Kopa na kundi lake la Ogopa Kopa angekuwepo kama tangazo lilivyosema, ni wazi kuwa mvua ile ingeshuka hata kabla ya Muumin kupanda jukwaani.

Maonyesho yote mawili yalidhidhirisha udhaifu kwa upande wa vyombo, hakukua na usikivu mzuri wa muziki, ingawa show ya El Clasico ilikera zaidi katika idara hiyo, ilifika wakati hata Muumin alijikuta akishutumu vyombo na kusema: “Hii ndio faida ya maandalizi ya kukurupuka”.

Katika wakati huu ambao bendi nyingi za dansi zinafanya maonyesho yao kwa kiingilio kinywaji, ipo haja ya waandaji wa El Clasico kulirudia onyesho lile katika ukumbi sahihi na kwa kiingilio sahihi. Kupeleka dansi Escape One kwa kutegemea majina ya wasanii badala ya majina ya bendi halafu kwa kiingilio cha sh. 15,000 ni ‘ujasiri’ uliopitiliza.


No comments