Habari

AYA 15 ZA SAID MDOE: AKUDO IMPACT NA MASHUJAA HAZIJAFA ILA ZINABADILISHIWA FIGO

on

Hakuna jambo gumu kama kutamka bendi fulani imekufa. Naam ni ngumu
kwasababu zinaweza kuwa zimekufa hadharani lakini bado zikawa hai BASATA.
Bendi zote zinasajiliwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na zinalipa
ada ya kila mwaka na huo ndio ‘uhai’ halisi wa bendi.
Bendi inaweza kukaa hata miaka mitano bila maonyesho, lakini bado
BASATA ikatambua uwepo wake kwa kuwa ni mwanachama hai.
Kama soko letu la muziki lingekuwa zuri na limerasimishwa kisasa, basi
bado bendi ingeweza kuingiza kipato kikubwa bila hata kufanya onyesho lolote
kwa mwaka mzima – mauzo ya nyimbo yangetosha kuleta neema.
Lakini kwa hali ilivyo na kwa namna soko letu lilivyo, mashabiki wengi
tunatambua uhai wa bendi kutokana na maonyesho yao ya kila wiki, kinyume na
hapo huwa tunaamini hiyo ni bendi mfu.
Hakuna mmiliki anayekuwa tayari kukiri kuwa bendi imekufa, siku zote
watakuambia aidha bendi ipo kambini au imesimamisha maonyesho kwa muda mfupi.
Kwao kusema bendi imekufa ni ‘uchuro’. Mfano mzuri ni bendi kubwa za
Akudo Impact na Mashujaa Band. Moja ipo kambini tangu Januari na moja
imesimamisha maonyesho ikisubiri vyombo vipya na haijafanya onyesho lolote la
maana mwaka huu huku kila mwanamziki akiwa anahaha kutafuta ugali wake kwenye
bendi zingine.
Kutokana na umakini wa wamiliki wa bendi hizi, usomi wao na pengine
hata uwezo wao wa kiuchumi, nalazimika kukubali kuwa bendi hizi hazijafa,
lakini nashawishika kuamini kuwa zipo mahututi hospitalini zikihitaji kubadilishiwa
damu au figo.
Naam bendi hizi zinahitaji kubadilishwa damu bila hivyo zitakufa kufa
kweli. Damu ya bendi hizi ni chafu na zimejaa virusi ambavyo ni hatari kwa uhai
bendi.
Nachelea kusema wamiliki wa bendi hizi ni ‘virusi’ kwa vile labda bado
ni mapema mno kusema hivyo, lakini sihofii kusema baadhi ya wanamuziki na
baadhi ya viongozi wa bendi hizi ni virusi vilivyosambaa kwenye damu ya bendi
na namna pekee ni kubadilisha damu.
Kama kiongozi wa bendi anakubali bendi isimamishe maonyesho kwasababu
ya uchakavu wa vyombo wakati kuna bendi kibao zinaishi kwa vyombo vya kukuodi, basi
kiongozi huyo ni kirusi. Mmiliki aliyekubali hatua hiyo naye anapaswa
kuchunguzwa pengine naye ni kirusi.
Kama kuna kiongozi anatengeneza mipango
ya bendi kukaa kambini kwa nusu mwaka bila onyesho lolote, bila kujali
wanamuziki wanaishi vipi, kiongozi huyo ni kirusi.
Kama wanamuziki wanakaa kwenye bendi kwa
zaidi ya mwaka mzima bila kutoa wimbo mmoja utakaoteka soko, huku wateja
wakiendelea kuyeyuka kwenye show zao, basi wanamuziki hao ni virusi. Kama
wamiliki wanashindwa kusimamia hilo, kama wanashindwa kuifanya bendi iwe na
japo video moja kali kwa mwaka, basi wamiliki nao ni virusi.
Na hapo ndipo ninaposema kuwa japo bendi
hizi mbili hazijafa, lakini zipo chumba cha wangonjwa mahututi, nyingine ikihitaji
kubadilishiwa damu, nyingine ikihitaji kubadilishiwa figo …kuna mstari
mwembamba sana kati ya uhai na kifo kwa bendi hizi.
Zipo bendi nyingi sana kwenye dansi na
taarab ambazo zipo kwenye hali hiyo, lakini nimelazimika kuzitaja Akudo na
Mashujaa kwa kuwa hakuna ubishi kuwa zilifanya makubwa kwenye muziki wa dansi,
ni hasara kwa jamii ya wapenda muziki iwapo bendi hizi zitapotea.

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *