BENCHI "LISILO NA SABABU" LAMSHANGAZA ABDI BANDA... asema mkataba wake ukimalizika Simba anasepa zake

BEKI wa Simba, Abdi Banda amesema kwamba hana tatizo la majeruhi kama watu wanavyosema na kwamba suala la nani apangwe kucheza ni jukumu la kocha mkuu, Joseph Omog.

Banda ambaye hivi karibuni alisimamishwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kosa la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavila tangu aachiwe huru ameshindwa kuitumikia timu hiyo katika mechi mbili za Ligi dhidi ya Azam na African Lyon.

Akihojiwa na mtandao mmoja wa michezo, Abdi Banda ambaye alikuwa akiwatazama wenzake wakisakata kabumbu dhidi ya African Lyon, amesema kitendo cha kutopangwa katika kikosi cha Simba kwa sasa haelewi nini shida ikiwa amekosa takriban mechi mbili ilihali hana majeruhi.

“Nafanya mazoezi na wenzangu lakini katika mechi zetu naambiwa wewe huna nafasi, ikiwa nipo fiti na wala sina majeruhi hata kidogo, mimi nashangaa na wala sijui chochote labda wewe ukamuulize kocha wangu Joseph Omog kwanini hanipangi katika kikosi?” amesema banda.

Banda amesema kuwa mkataba wake ukiisha msimu huu hana mpango wa kuongeza mkataba wake na Simba.
“Tayari nimeshasaini mkataba wa awali na timu moja ya Afrika Kusini ambayo ndiko nitakayojiunga nayo mara baada ya kumalizana na Simba,” amesema Banda.


Kiraka huyo mwenye uwezo wa kucheza beki namba 3, 4, 5 na kiungo namba 6, mzunguuko wa kwanza alitishia kuondoka katika timu yake hiyo kama angeendelea kufanywa mchezaji wa benchi.

No comments