BENKI YA NYIMBO ZA ISHA MASHAUZI INATISHA …ngoma kali kibao bado ziko kibindoni


KAMA kuna kitu kinamtia kizunguzungu Isha Mashauzi, basi ni ile hali ya kukata shauri ni nyimbo ipi atangulie kuiachia hewani kati nyimbo zake nyingi kali zilizoko kwenye maktaba yake.

Mwimbaji huyo anayeshikilia tuzo ya mwimbaji bora wa kike wa taarab, ana ngoma takriban tano ambazo zimeshakamilika na zote ni moto wa kuotea mbali.

Isha ambaye pia ameonyesha ubabe kwenye muziki wa rumba, tayari amerekodi nyimbo nne ukiwemo mmoja alioshirikiana na Christian Bella.

Nyimbo nyingine ni “Nibembeleze” ambao upo katika miondoko ya bongo fleva na dansi, “Utamu” na “Nitakonda” ambazo zimepigwa katika mchanganyiko wa aina yake uliojazwa ladha za taarab, chakakacha na zouk.

Lakini Isha pia ana nyimbo mbili kali za taarab alizoimba  kwaajili ya bendi yake ya Mashauzi Classic ambazo ni “Thamani ya Mama” na “Sudi Sudini”. Nyimbo hizi zimeshakamilika lakini bado hazijarekodiwa.

Isha ameiambia Saluti5 kuwa wimbo wa “Thamani ya Mama” utaingia kwenye albam ya “Kismet” huku “Sudi Sudini” ukiwekwa kiporo kwaajili ya albam itakayofuata baada ya “Kismet”.

No comments