BUKUNGU ACHEKELEA MAISHA SIMBA SC... atamani kucheza kikosi kimoja na Msuva, Mbaraka Yusuph, Mohammed Samatta na Aishi Manula

BEKI wa kulia wa Simba Janvier Besala Bokungu anafurahia maisha katika Simba na amekuwa rafiki wa wachezaji muhimu tofauti na alivyochukuliwa hapo awali.

Mkongwe huyo wa soka barani Afrika ambaye ni raia wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kwamba Tanzania ina vipaji lakini akawataja wachezaji watano ambao angependa kuwa nao katika kikosi kimoja.

Amesema kwamba pamoja na kuvutiwa zaidi na Ibrahim Ajibu ambaye anacheza nae katika kikosi cha Simba pia anavutiwa na kiungo mwingine mshamnbuliaji wa Yanga Simon Msuva.

Lakini pia Bokungu hakuficha mahaba yake kwa Mbaraka Yusuf ambaye anacheza Kagera Sugar huku ikidaiwa kwamba bado ni mchezaji halali wa Simba na kwamba amekwenda Bukoba kwenda kucheza kwa mkopo tu.

Beki huyo anayetumia akili nyingi uwanjani pia angependa kufanya kazi na kiraka wa Tanzania Prisons Mohammed Samatta ambaye ni kaka yake mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mbwana Samatta anayecheza katika kikosi cha KRC Genk ya Ubeligiji.

Lakini pia ukimuuliza Bokungu ni kipa gani angependa kuwa naye katika kikosi cha Simba basi kipa huyo simwingine dhaidi ya Aishi Manula anayecheza katika kikosi cha Azam FC.

“Wachezaji wapo wengi lakini hao ni baadhi ya ambao wananivutia kwa namna ambavyo wanacheza.”

Bokungu ni mchezaji aliyepata kucheza kwa mafanikio kwenye klabu za Esperance ya Tunisia na TP Mazenge ya Congo DR zenye majina makubwa kwenye Soka la Afrika.

Kwa sasa amekuwa "moyo" wa ulinzi katika safu ya ulinzi ya Simba akicheza kwa kujiamini na kufuta makosa ambayo yamekuwa yakifanywa na wenzake.

No comments