CANNAVARO ASEMA WAZAZI WAKE WALITAKA ACHUKUE KOZI POLISI ZANZIBAR BADALA YA KUJIUNGA NA YANGA

BEKI mkongwe wa timu ya Yanga, Nadri Haroub Cannavaro amesema kuwa ndoto ya kuichezea Yanga isingetimia kama wazazi wake wangeendelea kumshinikiza akajiunge na kozi ya polisi huko visiwani Zanzibar.

Nahodha huyo amesema kuwa alishajiunga na depo la polisi kabla ya Kamati ya usajili wa Yanga kumnasa juu kwa juu.

“Niweke wazi tu kuwa wazazi hawakutaka nijiunge na Yanga na walikasirika kusikia nakataa kwenda kujiunga na timu ya polisi Zanzabar kwasababu waliamini hata baada ya kuachana na soka nitakuwa mwajiriwa wa serikali,” alisema beki huyo.

“Maisha ya mpira ni mafupi kila mtu anajua, hilo lakini tangu nijiunge Yanga nimeweza kufanya mambo mengi makubwa na timu hii naiheshimu kwasababu najua imenitoa mbali,” aliongeza Cannavaro.

“Kuna mambo makubwa nimefanya na hata kuwa msaada kwa wazazi wangu. Kwasababu ya Yanga nimefikia hatua ambayo sidhani kama ningekuwa polisi ningeweza kuifikia.”

Beki huyo alimaliza kwa kusema kuwa ni kweli maisha ya soka ni mafupi lakini kama utatumia vizuri kipindi chako cha kucheza unaweza kupiga hatua kubwa sana.


Cannavaro ndiye mchezaji mkongwe zaidi ndani ya Klabu ya Yanga lakini hivi sasa amekuwa kwenye wakati mgumu baada ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.

No comments