CANNAVARO: INATUUMA SANA KUSHINDWA KUTETEA TAJI LETU LA FA DHIDI YA MBAO FC

NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub “Cannavaro” amesema imewauma sana kupoteza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mbao FC na kushindwa kutetea taji lao.

Cannavaro amesema hawakuyategemea matokeo hayo kutokana na uimara wa kikosi walichonacho ukilinganisha na kile cha Mbao FC.

“Sasa nimeamini kwenye soka kuna bahati, tumecheza muda wote langoni mwao lakini tukakosa bahati ya kuzitumia nafasi tulizopata nikiwemo mimi mwenyewe,” amesema Cannavaro.

Nahodha huyo amewapongeza Mbao FC kwa kucheza kwa nidhamu muda wote wa mchezo na kufanikiwa kulinda bao lao ambalo mchezaji wa Yanga, Vincent Andrew alijifunga katika harakati za kuokoa.

Cannavaro amesema, anatambua matokeo hayo yamewaumiza sana mashabiki wao lakini watahakikisha wanarudisha furaha yao kwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Vodacom.

“Tunawaomba radhi mashabiki wetu, naweza kusema tulikosa bahati kwa sababu tulishambulia sana lakini tulishindwa kuzitumia nafasi tulizozipata, tumekubali matokeo na tunawatakia kila la kheri katika mchezo wao wa nusu fainali,” amesema.


Yanga imerejea jijini Dar es Salaam jana ikijiandaa na mchezo wa Ligi ya Vodacom dhidi ya Kagera Sugar ambao utapigwa uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kesho Jumamosi, Mei 6.

No comments