DOGO MFAUME HATUNAYE TENA, MUNGU AILAZE ROHO YAKE MAHALI PEMA PEPONI

TAARIFA  za kifo cha aliyekuwa msanii wa mchiriku, Dogo Mfaume zimezidi kuthibitishwa na mmoja wa watu wake wa karibu ambaye pia ni msanii mwenzie wa miondoko hiyo, Kibabu Flavor.

Kibabu aliyeongea na saluti5 jioni hii, amesema kuwa Mfaume amefariki saa 9 alasiri, kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa katika taasisi ya mifupa (MOI) kwa zaidi ya wiki mbili sasa.

“Baada ya kuachana na matumizi ya dawa za kulevya, Mfaume alianza kukumbwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu ambapo hali ilivyoonekana kuwa mbaya alikimbizwa hospitali kwa matibabu,” amesema Kibabu.

Kibabu amesema kuwa, taratibu za mazishi ya Dogo Mfaume zitajulikana baadaye, ambapo kwa sasa anasubiriwa kaka yake aliyemtaja kwa jina moja la “Muddy” ambaye anakuja jijini Dar es Salaam akitokea Songea.

Wakati wa uhai wake, Mfaume ambaye ni kati ya wanafunzi wa marehemu Omary Omary, alitokea kujipatia umaarufu mkubwa, hasa kutokana na vibao vyake kadhaa vikali vikiwemo vile vitatu vya “Heleni”, “Kazi ya Dukani” na “Baba Mkwe”.   

Mungu ailaze roho ya marehemu Dogo mfaume mahali pema peponi. Amin.

No comments