FIFA YAAHIDI KUTOA "UAMUZI" KUHUSIANA NA RUFAA YA SIMBA YA POINTI TATU ZA KAGERA

NI kama Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), limezuia sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania baada ya kusema kwamba litatoa uamuzi kuhusiana na rufaa ya Simba.

Habari za uhakika ambazo saluti5 inazo ni kwamba FIFA tayari wameshatoa maelekezo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusubiri kwanza vikao mbalimbali ambavyo vitakaa kulingana na malalamiko ya Simba kisha kutoa uamuzi.

“FIFA wanataka kukaa kwanza wajiridhishe na kile ambacho Simba wanalalamika. Unajua Simba hawakupeleka jambo moja tu la Fakhi, kuna mambo mengi wamelalamika, sasa ngoja tuone itakuwaje,” kimesema chanzo chetu.

Imedaiwa kuwa Jumanne ijayo FIFA watapanga tarehe ya kusikiliza kesi hizo na huenda wakatoa uamuzi haraka katika muda mfupi ujao.

Juzi makamu wa rais wa klabu ya Simba, Geoffrey Nyange “Kaburu” amesema tayari wametuma malalamiko yao FIFA kuhusu pointi tatu walizonyang’anywa na TFF baada ya Kagera Sugar kumtumia mchezaji Mohammed Fakhi aliyekuwa na kadi tatu za njano walipocheza katika mechi ya Ligi dhidi ya timu hiyo ya Bukoba.

Kaburu amesema barua yao ya malalamiko imepokelewa na FIFA na wanachosubiri ni kusikia uamuzi gani utatolewa na Shirikisho hilo la Soka Duniani.

“Tumeshatuma malalamiko yetu na yamepokelewa FIFA , tumeainisha tunataka nini. Nisiwasemee, wao watasoma na wataamua halafu watatujulisha walichokiamua,” amesema Kaburu wakati akihojiwa jijini Dar es Salaam.


Simba walifikia uamuzi wa kupeleka jambo hilo FIFA baada ya Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji kutengua uamuzi wa Kamati ya masaa 72 ambayo awali iliipa Simba pointi tatu na magoli matatu baada ya kubaini ni kweli Kagera Sugar ilimchezesha Fakhi dhidi ya Simba huku akiwa na kadi tatu za njano kinyume na kanuni.

No comments