HUSSEIN MACHOZI ASEMA SYLVESTER MASHA NDIE ALIYEKATISHA MALENGO YAKE KISOKA

HUSSEIN Machozi amefichua kwamba aliyekuwa kocha wa timu ya Kagera Sugar, Sylvester Masha ndiye aliyekatisha malengo yake kisoka na kujikuta akiangukia kwenye muziki, baada ya kumpiga chini pamoja na wenzake wengine wawili na kuwapa nafasi wachezaji watatu wapya aliotua nao kutoka Mwanza.

Machozi amesema kuwa Masha aliingia Kagera Sugar na kumkuta akiwa chini ya kocha Mganda George Semugerere ambaye alikuwa anamwamini na kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza.

“Lakini alivyokuja Masha akiwa na wachezaji wake watatu ambao ni Mrisho Ngassa, Juma Jabu na Jumanne, ilibidi wachezaji wa zamani watatu waachwe ili wale aliokuja nao waingie, ndipo sisi tulipokutwa na bahati mbaya ya kuachwa,” amesema Machozi.

“Kwa upande wangu sababu ya kuachwa eti ilikuwa ni kwamba ningoje nikue kwanza eti sina nyama bado mdogomdogo, wakati nilikuwa niko sawa na nilikuwa nacheza vizuri tu.”

“Kwa vile nilikuwa niko mdogo sikuwa na maamuzi mazuri nikaamua kusema kwamba basi mimi kuanzia leo mpira basi, nikaacha kabisa. Nakumbuka kipindi hicho nilikuwa napigiwa simu sana na viongozi wa Yanga na Simba, lakini baada ya pale hata simu zao nikawa sipokei, nikawa sitaki tena.”

Machozi amekwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa matukio kama hayo yanawatokea wachezaji wengi sana hapa Bongo sio kwake tu, ambapo amedai kuwa soka la Tanzania lazima uwe na “refa”.

“Iwapo baba yako alikuwa mchezaji au mchika kibendera au hata mlinzi wa uwanja, ujue utacheza tu. Hata hao unaowaona timu ya taifa fuatilia historia zao, kuanzia golikipa mpaka namba 11 utakutana tu na mambo ya namna hiyo.”


“Lakini vipaji vya ukweli kabisa ambavyo hata ukimwangalia tu mtu unajua huyu soka lipo, huwa hawapati nafasi. Iko hivyo,” amesema Machozi ambaye hivi sasa anatikisa na kibao chake cha “Nipe Sikuachi”.

No comments