JAMES KOTEI ASUUZA ROHO ZA MASHABIKI WA SIMBA SC

KWA waliokuwa uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita wakati Simba ikicheza na Azam, watakuwa wameshuhudia kitu kimoja kikubwa.

Uwezo wa Mghana James Kotei kumdhibiti vilivyo mshambuliaji hatari wa Azam, John Bocco “Adebayor” kiasi kwamba nahodha huyo hakuweza kufurukuta.

Kotei ambaye ni kiungo, alicheza kama beki wa kati kukosekana kwa mabeki wawili mahiri; Method Mwanjali na Abdi Banda na hivyo Omog akaamua kumpanga Kotei ambaye alifanya kazi iliyowaacha midomo wazi mashabiki wote uwanjani.

Lakini hofu ya mashabiki wa Simba ilikuja pale Kotei alipopigwa kiwiko na Bocco na kuumia wakidhani kwamba asingerejea tena.

Omog alimsimamisha kinda Vicent Costa kupasha na mashabiki wa Simba wakaanza kuguna.

Ingawaje kinda huyo hakucheza lakini mmoja wa viongozi wa Simba alisema hakupandishwa kikosi cha wakubwa kwa bahati mbaya.

“Costa ni beki mwenye utulivu wa hali ya juu sana, anacheza kwa kujiamini na angecheza mashabiki mngebaki na mshangao,” amesema kiongozi huyo.

Amefichua kwamba tofauti na watu wengine wanavyofikiri, Costa ni beki mwenye uwezo wa hali ya juu na anakaba kiasi kwamba hampi mtu nafasi hata ya kupiga shuti.


“Kama angecheza mngeona tofauti yake na mabeki wengine hapa nchini, siku akibahatika kucheza mtaona kazi yake maana mazoezi anafanya vizuri sana,” alisema.

No comments