JANVIER BUKUNGU WA SIMBA ANUKIA KWA WATANI WAO YANGA MWISHONI MWA LIGI

USAJILI utakapoanza tu basi inawezekana Simba ikaumia vibaya baada ya beki wao mmoja na kiungo kukaribia kumwaga wino Yanga baada ya mazungumzo ya awali kukamilika kwa karibu kila kitu.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba beki atakayevaa uzi wa njano na kijani ni Mkongoman Janvier Bokungu ambaye anamaliza mkataba wake na klabu hiyo mara baada ya Ligi kumalizika huku akisemekana kuchoshwa na mikataba ya miezi sita ambayo amekuwa akipewa na timu hiyo.

Yanga itasajili beki mmoja wa kati mara baada ya zoezi la usajili kuanza kuchukua nafasi ya Vincent Bossou ambaye inaelezwa atahamia Vietnam mara baada ya msimu kumalizika ambapo Bokungu akiwa na uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa kati na huku pia akimudu kucheza kama beki wa kulia.

Mbali na Bokungu, pia Yanga inakaribia kumnasa kiungo Said Ndemla ambaye pia mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu ambaye tayari amebakiza hatua chache kusajili fomu za usajili za timu hiyo huku akionekana kumvutia kocha wa timu hiyo George Lwandamina ambaye ametaka kusajiliwa kiungo mchezeshaji.

Wawili hao tayari inasemekana wameshafanya mazungumzo ya awali na mabosi wa klabu hiyo huku sasa wakisubiriwa kusaini mikataba ya awali katika timu hiyo.

“Bokungu unajua mkataba wake unamalizika msimu huu lakini tumeongea na mwakilishi wake, amesema anataka kuondoka na kutafuta changamoto nyingine na hana tatizo hata la kuja hapa kwetu, tumeshaweka sawa kila kitu, kuna mambo yakikaa sawa tunamaliza,” alisema bosi huyo wa Yanga.


“Unajua uzuri wa Bukungu nafasi zote za beki anacheza, sasa tunataka watu wa namna hiyo, lakini mbali na huyo pia tunamtaka yule Ndemla, tushazungumza nae na kila kitu kinakwenda sawa.”

No comments