JUDO TAIFA WAENDELEA NA KAMBI YA MAZOEZI KUJIANDAA NA MASHINDANO YA KIMATAIFA

CHAMA cha Judo Tanzania (JATA) kinaendelea na mikakati ya kuiandaa timu ya taifa ya mchezo inayojiandaa na mashindano yajayo ya kimataifa huku kukiwepo na changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukitafutia kikosi hicho mechi za kirafiki.

Kikosi cha timu ya taifa ya judo kinajiandaa na mashindano ya dunia yanayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Akizungumza na saluti5 Katibu mkuu wa chama hicho, Innocent Mally amesema hatua ya mkakati huo ni kutaka kutimizwa kwa malengo ya timu hiyo kwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Alisema, mkakati wa chama chake ni kuhakikisha timu inapata mapambano ya kirafiki ingawa changamoto ya ukosefu wa fedha ikiikabili JATA.

“Kwa kweli chama kinatamani sana timu ipate mechi za kirafiki za kimataifa kwa ajili ya vijana wetu waweze kujua mapungufu na yaweze kufanyiwa kazi kabla ya kuelekea katika mashindano yaliyopo mbele yetu,” alisema Mally.

Aliongeza kuwa kwa sasa wachezaji wameteuliwa katika kikosi cha taifa  na wanaendelea na mazoezi huku chama kikipambana kwa ajili ya kusaka fedha za kuisafirisha timu ifikapo muda wa kwenda katika mashindano.

Mally alisema kuwa chama kilitamani kuweka mikakati ya kuandaa timu kupata mechi za ndani na nje ya nchi ili kuimarisha kikosi kabla ya kuelekea katika mashindano makubwa ya kimataifa.


Akielezea maendeleo ya sasa alisema kuwa timu inaendelea na kujiwinda chini ya kocha wao wakati wa kusubiri kufanya mchujo kupata idadi ya washiriki kulingana na kiasi kitakachopatikana cha pesa kitakachowawezesha kusafirisha timu hiyo.

No comments