JUDO TANZANIA WATEMBEZA BAKULI KWA AJILI YA KAMBI YA MAANDALIZI YA TIMU YA TAIFA

CHAMA cha Judo Tanzania (JATA), kinatafuta fedha kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya timu ya taifa inayotarajia kushiriki mashindano ya dunia mwaka huu.

Kutokana na jukumu hilo, Katibu mkuu wa JATA, Innocent Mally ametoa wito kwa wadau kutoa sapoti ya kufanikisha ili kuweza kupeleka vijana katika mashindano hayo ya kimataifa.

Alisema kuwa kwa sasa vijana hao wanaendelea na kambi ya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo.

Mally alisema kuwa kikosi kimechaguliwa lakini fedha itakayopatikana itawezesha kujua idadi ya wachezaji watakaokwenda kushiriki mashindano hayo.

“Sisi malengo yetu ni kuhakikisha vijana wanajiandaa vyema ili wakaipeperushe bendera na ili kuweza kutoa morari ni Watanzania kujitokeza kutusapoti na kutuunga mkono kuweza kufikia malengo yetu,” alisema Mally.

Katibu huyo alisema kuwa kiu ni kuhakikisha wanapatikana wachezaji wa uzito wa awali hadi wa juu kwa ajili ya uwakilishi katika mashindano hayo.


Aliongeza kusema kuwa vijana wana ari na morari ya kushiriki kimataifa hivyo shime Watanzania kuungana kwa pamoja kuweza kusukuma gurudumu hilo kwa maendeleo zaidi kupitia mchezo huo.

No comments