JUVENTUS YA ITALIA KUTUA SIMBA SC MWEZI UJAO

SIMBA wameamua kufanya kweli katika kuiendesha klabu yao katika hali ya kisasa zaidi kulinganishwa na timu nyingine za hapa nchini.

Awali kulikuwa na habari kwamba Simba inakaribia kuingia makubaliano na klabu bingwa ya Italia, Juventus, lakini sasa habari hizo zimefikia hatua mpya.

Baada ya kusaini mkataba na kampuni ya Sportpesa ya Kenya kuidhamini Simba, sasa wekundu hao wanakaribia kuvuna mkwanja mnene zaidi kutoka kwa miamba hao wa Italia.

Saluti5 imechungulia kwenye “chumba cha siri” cha Simba na kugundua kwamba wekundu hao wako katika mazungumzo muhimu na Juventus na huenda wakurugenzi wa klabu hiyo tajiri barani Ulaya wakatua nchini mwezi ujao.

Habari hizo zinasema kwamba Juventus wanakuja kwa mwaliko wa mfadhili wa klabu hiyo, Mohammed Dewji “Mo” ambaye alifanya nao mazungumzo ya awali nchini Italia hivi karibuni alipokuwa huko kibiashara.

“Mo ndie anayewaleta Juventus na kisha atawakabidhi kwa viongozi wa Simba. Pamoja ma mengine, wanakuja kuangalia namna ya kuwekeza katika klabu hii ikiwa ni pamoja na kuanzisha timu ya watoto wa umri kati ya miaka 12 na 15, kisha kuona namna ya kuwekeza katika uwanja wa Bunju ambao Simba wanaujenga,” kimesema chanzo chetu.

Chanzo hicho kimesema kwamba mipango ya Simba ni kuwa na watoto kuanzia miaka 12 ambao watakuwa katika vikosi mbalimbali kwa ajili ya maslahi ya Simba na taifa baadae.

Mo alikaririwa akisema kwamba ameshafanya mazungumzo na uongozi wa Juventus na kilichosalia ni viongozi wa Simba kumalizia hatua iliyobaki.

No comments