KICHUYA AWEKA NADHIRI DHIDI YA MBAO FC MCHEZO WAO WA FAINALI

KIUNGO mshambuliaji wa Simba Shiza Ramadha Kichuya ni kama ameweka nadhiri dhidi ya Mbao FC ya Mwanza katika mchezo wa fainali wa kombe la shirikisho utakaochezwa mwishoni mwa mwezi huu mjini Dodoma.

Amesema kwamba dhamira yake ni kuwafunga Mbao na amepania kuibeba timu yake katika mchezo huo muhimu akisema ameshawajua pakuwapigia.

Kichuya amesema amejipanga kucheza kwa kujituma kwa sababu hiyo ndio itakuwa shukrani yake pekee kwa timu yake na kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili waweze kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.

“Nitafurahi sana kama nitafunga bao la kuipa ubingwa wa FA timu yangu kwa sababu tumekuwa na msimu mzuri lakini mwishoni umeonekana mgumu kutokana na kila timu ambayo tunapambana nayo inakuwa inatupania kusababisha kupata matokeo ambayo hayaturidhishi,” amesema Kichuya.

Amesema kwa sasa yupo fiti na kiwango chake kimezidi kupanda siku hadi siku hivyo ana uhakika wa kupata nafasi kwenye kikosi kitakachoanza mchezo huo na yupo tayari kujitoa kwa ajili ya timu yake.

Kichuya amesema amecheza na Mbao mara mbili na amewajua vizuri mapungufu yao hivyo atahakikisha anayatumia kwa kuwafunga ili kusaidia timu yake kupata nafasi ya kushiri michuano ya kimataifa mwakani.

Amesema, hakuna linaloshindikana ingawa Mbao ni timu ngumu na iliwasumbua kwenye mechi zote mbili walizocheza kabla ya mchezo huu wa fainali lakini wamejipanga kucheza kufa na kupona ili kutwaa taji hilo.


“Fainali hii ni muhimu sana kwetu na tunahakikisha tutawapa raha wapenzi wetu kwa kuchukua Kombe hilo, hivyo nitapambana kuhakikisha timu yangu inashinda na kila mchezaji analijua hilo hivyo hatutafanya mzaha kila mmoja atacheza kwa kujituma akijua fika nini tunachotakiwa kufanya,” alisema.

Simba imepata tiketi ya kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya kuichapa Azam bao 1-0, katika mchezo uliochezwa Jumamosi iliyopita kwenye uwanja wa Taifa,Dar es Salaam, wakati Mbao ilipata ushindi kama huo dhidi ya Yanga kwenye mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.

No comments