KIPA DANIEL AGYEI ALETA UTULIVU KWA MASHABIKI WA SIMBA SC


UNAWEZA kusema kwamba walau katika siku za hivi karibuni wanachama na mashabiki wa Simba wamekuwa watulivu mara baada ya kusajiliwa kwa kipa Mghana Daniel Agyei kwenye kipindi cha dirisha dogo.

Hatua hiyo ilifanywa baada ya kutokuwa na imani na aliyekuwa kipa namba moja wa kikosi hicho raia wa Ivory Coast, Vincent Angban ambaye walidai alikuwa akifungwa magoli mepesi mno.

Hata hivyo, Agyei ameonekana kutibu tatizo hilo ingawa kwenye mechi za karibuni amekuwa akitatizwa na kukosekana kwa beki Method Mwanjali, hivyo kuruhusu magoli kutokana na uzembe na makosa ya mabeki wake.

Alishawahi kucheza mechi zaidi ya sita bila kuruhusu goli wakati beki ikiwa imara chini ya Mzimbabwe Mwanjali.
Anahesabika kuwa mmoja wa makipa aliyetamba msimu huu na habari zinasema kwamba miongoni mwa makipa watano wanaowania tuzo ya kipa bora, Agyei ni mmoja wao.


Habari zinasema kwamba Mghana huyo anaweza kuwa kipa bora wa Ligi Kuu ingawa anakabiriwa na ushindani kutoka kwa Aishi Manula wa Azam FC, Juma Kaseja wa Kagera Sugar na Deo Munishi wa Yanga.

No comments