KIPA WA SIMBA AANZA KUIGWAYA MBAO FC... asema washambuliaji wa Mbao wana kasi ya "kutisha" uwanjani

KIPA namba moja wa Simba, Daniel Agyei raia wa Ghana ameonekana kuonyesha wasiwasi katika mchezo wao wa fainali dhidi ya Mbao FC  ya jijini Mwanza ambapo watakumbana kuwania ubingwa wa Kombe la FA.

Mlinda mlango huyo alisema kwamba inawapasa kucheza kwa tahadhari kubwa katika mchezo huo wa fainali kutokana na kasi waliyonayo washambuliaji wa timu ya Mbao.

“Najua ugumu wa kucheza na Mbao FC. Sio timu ndogo kama inavyodhaniwa, ni lazima tucheze kwa tahadhari kubwa kwenye hatua ya fainali,” alisema kipa huyo.

“Mechi ya fainali haijawahi kuwa rahisi, hasa unapopambana na timu zenye kawaida ya kupania mechi, ni lazima uwe makini zaidi,” aliongeza kipa huyo.

Simba inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuruhusu mabao mawili katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao ambao ulichezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mchezo huo wa fainali unatarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Mei 28, mwaka huu ambapo ilishindikana kwa mchezo huo kupigwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kama ambavyo imezoeleka kwa sababu Simba watakuwa na faida ya kuwa mwenyeji.


Bingwa wa mchezo huo atapata tiketi ya kushiriki kwenye michuano ya Kombe la CAF na ikiwa Mbao itafanikiwa kuibuka na ushindi itakuwa imejiandikia historia ya kupanda daraja na kushiriki moja kwa moja kwenye michuano ya kimataifa.

No comments