KIUNGO WA MBAO FC ASEMA YUKO TAYARI KUTUA SIMBA SC

KIKOSI cha Mbao FC kinaundwa na vijana machachari wenye uthubutu wa kupigana muda wote na ndio maana wamefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la FA.

Mmoja wa vijana hao machachari ni kiungo Salmin Hoza ambaye ana uwezo mkubwa katika dimba la kati na sasa ameanza kuona mwanga wa kutaka kujiunga na Simba.

Hoza ambaye katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Yanga kwenye uwanja wa CCM Kirumba, aliwafunika kabisa Said Makapu na Kamusoko katika eneo la kati, amesema yuko tayari kujiunga na Simba kama watamtaka.

Salmin amesema hawakuwa na hofu na Yanga hata kidogo na walijiamini sana katika mchezo huo na ndio maana walionekana kuwamudu Yanga muda mwingi wa mchezo.

Amedai, Yanga walikuwa wa kawaida sana lakini tatizo kubwa hasa kwake lilikuwa ni Haruna Nyionzima ambapo anakiri alishindwa kumkaba Mnyarwanda huyo.  

“Nimekutana na viungo wengi wa Ligi Kuu Tanzania, wengi wana udhaifu na uimara wao, lakini mara zote Nyionzima nimeshindwa kujua udhaifu wake na ananipa taabu sana,” amesema Salmin.

Hata hivyo kiungo huyo amekiri kwamba anawindwa na Simba na hata Yanga lakini akasema kwamba kwa sasa anaangalia maisha yake katika kikosi cha Mbao, ingawa amesema akimaliza mkataba wake lolote linawezekana.


Simba imekuwa ikimwania kiungo huyo pamoja na nahodha wa Mbeya City, Kenny Ally ili kuimarisha safu yake ya kiungo ambayo huenda ikawapoteza baadhi ya viungo wake wanaowania kwenda nje ya nchi.

No comments