KOCHA WA STARS AWASHANGAA WANAOBEZA KUITWA KIKOSINI KWA THOMAS ULIMWENGU

KOCHA wa timu ya Taifa Stars, Salum Mayanga anashangaa watu wanaobeza kuitwa kikosini kwa mshambuliaji Thomas Ulimwengu ambaye anacheza soka la Kimataifa kwenye klabu ya AFC Eskilstuna ya nchini Sweden.

Kocha huyo alisema kuwa hakufanya uamuzi huo kwa kurupuka kwani tayari alishafanya mazungumzo naye ili kujua mwenendo wake nchini Sweden.

“Nilifanya mazungumzo naye siku tatu kabla ya kumwita kwenye kikosi cha timu ya Taifa lakini pia nilipata muda wa kuzungumza na viongozi wa klabu yake,” alisema kocha huyo.

“Nilisharidhika na hali yake baada ya kuelezwa ameanza mazoezi siku 10 nyuma na hata uchunguzi wa goti lake yuko vizuri kwa ajili ya kucheza,” aliongeza kocha huyo.

Nyota huyo hakuwepo kwenye kikosi cha Stars kwa muda mrefu tangu apate jeraha la goti na hata kwenye klabu yake ya sasa amekuwa nje ya kikosi kwa sababu ya tatizo hilo la goti.

Baadhi ya wadau wa soka wameshangaa uamuzi wa kocha huyo kumjumuhisha kikosini Ulimwengu ambaye amekuwa akiwekwa benchi kwa muda mrefu kutokana na jeraha la goti.


Mashabiki wa soka wamekuwa wakituma maoni mbalimbali kwa njia ya mtandao wakishangaa kuitwa Thomas ambaye ana siku 10 tu za mazoezi.

No comments