KUKOSEKANA TIMU ZA NJE KWAONDOA MSISIMKO NGUMI ZA RIDHAA DAR

CHAMA cha ngumi za Riadha mkoa wa Dar es Salaam (DABA) kimesema ushiriki wa timu za nje katika mashindano ya nne ya kuwania Kombe la mastahiki meya wa jiji la Dar es Salaam umechangia kutokuwa na ushindani mkubwa kulingana na mwaka jana.

Mwaka jana timu kutoka majiji mbalimbali ya nje ya nchi ziliweza kuleta wachezaji wake na kuchangia kuongeza changamoto kwa vijana wa ndani waliopata fursa ya kushiriki na kuweza kujifunza na kujipima viwango vyao.

Akiongea na saluti5, Katibu mkuu wa DABA, Wamboi Mangore alisema kuwa kila mwaka chama kinatoa mialiko mbalimbali kwa majiji ya ndani na nje ya nchi yaweze kuungana kwa pamoja kwa lengo la kudumisha ushirikiano kupitia michezo.

Alisema kuwa, mwaka huu timu ya nje mwaka huu imekuja ya Mombasa nchini Kenya ambayo imeleta mchezaji mmoja na wengine ni klabu za jiji la Dar es Salaam.

Mangore alisema kuwa lengo la kushirikisha timu za nje katika mashindano hayo ni pamoja na kuhakikisha wachezaji wa ndani wanapata ushindani katika michezo na kushirikiana na kupeana changamoto za michezo kwa vijana.

Katibu huyo alisema kuwa, licha ya timu za nje kutokuja, bado vijana walioshiriki katika mashindano ya mwaka huu wameonyesha morari ya kupenda michezo.

“Kwa kweli tulitegemea kupata timu kutoka nchi mbalimbali ambazo tunashirikiana nazo lakini hazijaweza kuja kwa mwaka huu, lakini tunashukuru mashindano yetu yameenda vizuri na vijana wameonyesha morari kubwa sana,” alisema Mangore.

Alisema kuwa, timu zilizoshiriki ni 13 ambazo ni pamoja na Magereza A, B, C, MMJKT, Mbweni JKT, Ruvu JKT, Chang’ombe JKT, Mgulani JKT, Mzizima, Dar City, Manispaa ya Ubungo, Kinondoni na Kigamboni.

No comments