LIVERPOOL YAUA 4-0 NA KUIKATA MAINI ARSENAL ‘TOP FOUR’ … Hull City nayo yashushwa daraja


Liverpool imeichapa West Ham 4-0 na kufikisha pointi 73 ambazo zinaisogeza karibu kwenye kunasa  tiketi ya ‘top four’ ya Premier League, hatua ambayo inaiweka pabaya Arsenal yenye pointi 69.

Liverpool ipo nafasi ya tatu na imebakisha mchezo mmoja huku timu pekee zinazoweza kuifikia ni Manchester City yenye pointi 72 na michezo miwili mkononi na Arsenal ambayo pia ina michezo miwili.

Arsenal sasa imebakiwa na nafasi finyu ya kumaliza nafasi ya nne ambapo itabidi ishinde mechi zake mbili zilizobakia ili kufikisha pointi 75 kuziombea mabaya City na Liverpool.

Manchester City ambayo inaizidi Arsenal kwa wasatani wa magoli matano, inaweza ikahitaji pointi tatu tu ili isifikiwe na Arsenal.

Mabao ya Liverpool yamefungwa na Daniel Sturridge, Divock Origi na Philippe Coutinho aliyefunga mara mbili.

Wakati huo huo Hull City imeungana na Middlesbrough na Sunderland kuagana na Ligi Kuu ya England baada ya kufungwa 4-0 Crystal Palace.


No comments