MANCHESTER UNITED NA AJAX ZATINGA FAINALI KWA MBINDE ...Eric Bailly alambwa red card


Manchester United imetinga kwa mbinde fainali ya Europa League baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Celta Vigo ya Hispania.

Kama Celta Vigo wangepata bao la pili Old Trafford, basi United ingekomea nusu fainali licha ya kushinda 1-0 katika mchezo wao wa kwanza wiki iliyopita.

United walipata bao la kuongoza dakika ya 17 kupitia kwa Fellaini ambaye aliunganisha kwa kichwa krosi ya Rashford na kudumu hadi dakika ya 85 pale Facundo Sebastian Roncaglia alipoisawazishia Cetla Vigo.

Kikosi cha Mourinho kinakwenda fainali kikiwa na hasara ya kumkosa beki tegemeo Eric Bailly aliyepewa kadi nyekundu dakika ya 88 baada ya kumpiga kibao John Guidetti, hatua iliyoleta mzozo uliopelekea Roncaglia wa Celta Vigo  naye pia apewa kadi nyekundu katika tukio hilo.

Wakati United ikipenya fainali kwa mbinde, Ajax nayo ilikuwa na msukosuko mkubwa baada ya kulambwa 3-1 na Lyon, lakini wakafanikiwa kutinga fainali kwa jumla ya bao 5-4 kufuatia ushindi wa 4-1 kwenye mchezo wa kwanza.

Fainali itapigwa Jumatano Mei 24 kwenye dimba la Friends Arena huko Stockholm, Sweden. 
  

No comments