MANJI AWATIA MZUKA WACHEZAJI YANGA KWA AHADI NONO ZA MALIPO YA MISHAHARA NA POSHO

YANGA ni kama vile tayari imeshawanyamazisha watani wao Simba kwa hatua ya kutangaza ubingwa rasmi Jumanne lakini kuelekea kumaliza mechi mbili za mwisho, mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuph Manji amewatia mzuka wachezaji akiwapa ahadi nono.

Taarifa kutoka ndani ya kikosi cha Yanga ni kwamba Manji amewataka wachezaji wa timu hiyo kupambana kwa nguvu katika kumalizia Ligi huku akiwataka kuhakikisha wanashinda mpaka mchezo wa mwisho dhidi ya Mbao, 
kesho Jumamosi Mei 20 pale CCM Kirumba jijini Mwanza.

Katika taarifa yake hiyo, Manji anaelezwa amewapa ahadi kubwa wachezaji wa timu hiyo kwamba anataka kumaliza tatizo lao la mishahara huku akiwapa ahadi nyingine ambayo imewatia mzuka zaidi.

“Mwenyekiti yupo pamoja na timu ila hataki kufanya mambo yake kwa mazoea, ameongea na wachezaji na hivi karibuni amewaambia hakuna kitu kitakachopotea katika haki zao, mishahara yao watapatiwa na mambo yote,” alisema bosi huyo.

“Unajua wachezaji wetu walivyo kama wasingekuwa wamepewa pochi halisi ya malipo yao wasingejituma kama hivi katika mechi hizi tatu lakini kupambana kwao kote huko ni kutokana na mazungumzo yao na mwenyekiti ambapo yamewatia mzuka.

Katika kujipanga na mchezo wa Mbao, Yanga imedhamiria kuishusha daraja timu hiyo ambapo vigogo wa Kamati ya mashindano wanatangulia jijini Mwanza leo kuhakikisha hakuna makosa yatakayofanyika katika mchezo huo wa mwisho lengo likiwa ni kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA.

No comments