MBARAKA YUSSUF WA KAGERA SUGAR AIDENGULIA SIMBA SC... anukia kutua Yanga "mdogomdogo"

STARAIKA wa Kagera Sugar, Mbaraka Yusuf amefanya maamuzi yatakayowaumiza viongozi wa klabu yake ya zamani ya Simba, baada ya kugoma kupokea simu za vigogo wa timu hiyo huku pia rafiki zake wakivujisha kwamba hana kinyongo kutua upande wa pili, Yanga.

Taarifa kutoka ndani ya Kagera Sugar ni kwamba licha ya kujua kuwa Simba kupitia mwenyekiti wa Kamati ya usajili iliyo chini ya ZachariaHans Poppe wamekuwa wakimpigia simu mshambuliaji huyo kinda lakini amekuwa hataki kurudi kwenye klabu hiyo.

Wakati Simba ikipambana hivyo rafiki mmoja wa mshambuliaji huyo amefichua kuwa Yanga imetupa ndoano kwa Mbaraka ambapo kinda huyo ameonyesha hana kinyongo katika kuvaa jezi ya njano na kijani endapo maslahi yatafikiwa.

Rafiki huyo amesema Yanga imeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo aliyebakiza mkataba wa mwaka  mmoja na Kagera Sugar endapo hataongeza na Mbaraka amekubali kuhamia katika klabu hiyo baada ya kusemekana kuchoshwa na ubabaishaji wa Simba akitaka kucheza Ligi ya Mabingwa.

“Simba hawataweza kumpata tena Mbaraka, unajua jamaa amewachukia kwa usumbufu waliomfanyia katika mkataba wake lakini Yanga wakijipanga vizuri wanaweza wakampata kirahisi sana ingawa ana mkataba na Kagera wa mwaka mmoja,” alisema rafiki huyo.


“Mbaraka anataka maslahi mazuri na mambo yaliyonyooka hataki longolongo za Simba, Yanga wamemfuata lakini urahisi kwao ni kucheza mechi za kimataifa ambayo ndiyo kiu yake sasa.”

No comments