MBWANA SAMATTA ANUKIA WOLFSBURG UJERUMANI MWISHONI MWA MSIMU

NAHODHA wa timu ya Taifa, Mbwana Samatta ambaye anachezea timu ya Genk ya nchini Ubelgiji, anaweza kutimka kwenye klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu baada ya klabu kadhaa za ujerumani kuonyesha nia ya kuitaka saini yake.

Timu za Wolfsburg na Hamburger za nchini Ujerumani zimeripotiwa kufuatilia mwenendo wa Samatta tangu wakati wa michuano ya Kombe la Europa ambapo walitolewa na Celta Vigo ya Hispania kwenye hatua ya robo fainali.

Thamani yake sokoni inakadiriwa kufikia euro mil 10 baada ya kuifikisha timu yake kwenye hatua ya robo fainali kwenye Kombe la Europa huku akitumika kwa dakika zote 90 za mchezo.

Hata kama uhamisho huo hautafanikiwa mwishoni mwa msimu huu, bado mshambuliaji huyo ana nafasi ya kushiriki kwenye michuano ya Europa mwakani baada ya juzi timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo dhidi ya Kortrijik.

Katika mechi hiyo ya kuwania kufuzu michuano ya Ulaya, Samatta aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Leandro Trossard aliyefunga bao la kwanza kwa njia ya penati.

Genk inatarajia kutengeneza faida kubwa kupitia mgongo wake kwani ilimnunua kutoka TP Mazembe ya Congo DRC kwa euro 800,000.

No comments