MECKY MAXIME AJITAPA: "NIKITUA YANGA NITAWALETA KICHUYA, MUZAMIR NA MO WAPYA"

YANGA inatarajia kufanya maamuzi magumu ya kumchukua kocha Mecky Maxime lakini mwenyewe ametangaza utamu kwamba akitua klabu hiyo itavuna vipaji vingi kutoka katika jicho lake.

Akiongea na saluti5, mmoja wa vigogo wa Kamati ya usajili amesema katika kikao cha awali na kocha huyo kijana mwenye mafanikio, amewaambia kwamba endapo watakamilisha haraka mchakato wa kumchukua, Yanga itanufaika na kazi yake ya kuvumbua vipaji.

Bosi huyo amesema Maxime amewahakikishia kwamba anajua wapi vinapatikana vipaji bora ambapo Yanga itakuwa bora zaidi kwa kuwapatia wachezaji wapya wenye uwezo zaidi ya Shiza Kichuya, Muzamir Yassin na Mohammed Ibrahim “MO” wanaotamba Simba wakitoka katika uvumbuzi wake.

Aidha bosi huyo amesema ujio wa Maxime ndani ya Yanga utaambatana na usajili wa mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mbaraka Yusuph ambaye nae anatakiwa na kocha George Lwandamina.

“Tunamtaka kweli Maxime, unajua sisi tunataka kufanya maboresho makubwa katika benchi letu na jicho letu limetua kwa Maxime na tulitaka kumchukua mapema lakini tulisitisha mpango huo kwa muda,” alisema bosi huyo.


“Tumekutana na Maxime mwenyewe, hana shida katika kutua hapa na ametuambia kwamba anajua Yanga inayumba wapi katika kupata wachezaji wazuri na akitua hapa kazi hiyo ataifanya yeye kwa kumuonyeshwa Lwandamina wachezaji bora.”

No comments