METHOD MWANJALI SASA YUKO FITI ILE MBAYA... ajiandaa na michuano ya Sportpesa

BEKI kisiki wa Simba raia wa Zimbabwe, Method Mwanjali yuko fiti tofauti na watu wengine wanavyodai.

Mwanjali ambaye amekuwa majeruhi kwa muda mrefu, sasa imebainika kwamba amepona kabisa na atakuwa katika mechi zote za michuano maalum ya Sportpesa inayoanza mapema mwezi ujao.

Katika mazoezi ya Simba yaliyokuwa yanaendelea mjini Dodoma kabla ya mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mbao FC, Mwanjali alikuwa fiti kabisa na kulikuwa na fununu kwamba angepangwa juzi.

Hata hivyo, kocha wa Simba, Joseph Omog ameamua kumuweka akiba mchezaji huyo kwa ajili ya michuano hiyo ambayo itazishirikisha timu nne kutoka Tanzania na nyingine nne kutoka nchini Kenya.

Tangu kuumia kwa beki huyo, ukuta wa Simba umekuwa ukiyumba kwa kiasi kikubwa na kumfanya Omog kumtumia kiungo raia wa Ghana, James Kotei kukamata nafasi ya Mwanjali.

Lakini pia kiongozi mmoja wa Simba amekanusha habari zinazoendelea kwenye mitandao kwamba Simba wanataka kuachana na beki huyo.

Kiongozi huyo amesema kwamba Simba haina mpango wa kumuacha Mwanjali na kwamba bado yuko kwenye mipango ya muda mrefu katika kikosi cha Omog.

“Kuna watu wanasambaza habari kwamba Mwanjali anaachwa. Habari hizi sio za kweli kwasababu kocha wetu amemuweka Mwanjali katika mapendekezo yake ya kikosi kijacho,” amesema.  
 

No comments