MO ATAKA MIKATABA MIPYA YA MKUDE, BANDA NA AJIB MPYA MSIMBAZI

MFADHILI wa Simba, Mohammed Dewji “Mo” ameingilia kati nafasi ya viraka wa timu hiyo, Abdi Banda, Ibrahim Ajib na nahodha Jonas Mkude.

Habari za uhakika zinasema kwamba Dewji amesikia kuwa wachezaji hao wanaondoka baada ya kumaliza mikataba yao lakini amesema kwamba Simba ya sasa ina malengo makubwa na si ya kuwaacha wachezaji wazuri kuondoka.

Ni kutokana na umuhimu wao baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, Mo anadaiwa kuwaita wachezaji wote wanaomaliza mikataba ili kumalizana nao wabaki Simba.

Banda ambaye mkataba wake umemalizika, alikuwa anatajwa kutimkia nchini Afrika Kusini lakini Mo amemzuia kuondoka.

Habari zinasema kuwa mfadhili huyo amemwita Banda kwenda kumsikiliza na kumalizana nae leo Jumatatu ili abaki Simba.

Lakini pia habari zinasema kuwa, mwanachama na mfadhili huyo wa simba amewaita ajib na Mkude na ameshawaambia viongozi wa klabu waandae mikataba na wachezaji hao.

“Unajua Mo ana mikakati mikubwa katika Simba, hataki kusikia habari kwamba eti wachezaji wazuri wanaondoka, akili yake ni kwamba anataka kuona wachezaji wazuri wanakuja Simba,” kimesema chanzo kimoja.


Chanzo hicho kimesema kwamba wachezaji hao watapewa kila mmoja mkataba wa miaka miwili ingawaje kutakuwa na kipengele cha kuwaruhusu kuondoka kama watapata timu za nje ya nchi kwa nia ya kuwaendeleza zaidi.

No comments