MPIRA WA WAVU WAMWOMBA MSAJILI WA VYAMA KUTOA KIPAUMBELE CHA USAJILI KWA VYAMA VYA MIKOA


CHAMA cha mpira wa wavu Tanzania (TAVA), kimemwomba msajili wa vyama vya michezo kutoa kipaumbele kwa kusajili vyama vya mikoa vya mchezo huo vilivyowasilisha maombi yao.

Wito huo uliotolewa na mwenyekiti  wa chama hicho, Augustino Agapa ambaye alisema kuwa lengo ni kuhakiki vyama hivyo vinapata usajili na viweze kufanya usajili wa mkoa ili kupata fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu wa taifa utakaofanyika Julai 8, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa hadi sasa tayari kuna zaidi ya mikoa 15 ambayo imepeleka maombi kwa msajili kwa ajili ya kupata usajili katika vyama vya mikoa yao ambapo baadhi ya mikoa imeshakamilisha.

Agapa alisema kuwa, sanjali na hilo TAVA inasisitiza vyama vya mikoa kuhakikisha vinakamilisha usajili wa vyama vyao pamoja na kufanya uchaguzi ili kuweza kupa kibali cha kushiriki uchaguzi mkuu wa taifa.

‘Tunaomba msajili kutoa kipaumbele kwa ajili ya kusajili vyama vilivyoomba kusajili vyama na kutokana na mwitiko wa kusajili vyama kuwa mkubwa, matarajio yetu itakapofika muda wa uchaguzi vyama vingi vitapata fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu wa taifa,” alisema Agapa.

Lakini pia mwenyekiti huyo alisema kuwa changamoto iliyopo sasa ni vyama vingi vya mikoa kuwa havijafanya uchaguzi pamoja na baadhi yao kutosajiliwa hadi sasa.


Alifafanua kuwa kutokana na hali hiyo ya kutokamilika kwa baadhi ya mambo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), lilichukua hatua ya kutoa muda wa maandalizi ya uchaguzi mkuu ili vyama vya mikoa ambavyo havijakamilisha viweze kukamilisha.

No comments