NIKKI WA PILI ALIVYOPIMANA UBAVU NA BASATA KWENYE MEZA HURU YA ITV


Msanii nyota wa hip hop hapa Tanzania, Nikki wa Pili, Ijumaa iliyopita alionyesha ubingwa wa kujenga hoja pale alipoitwa na ITV kwenye kipindi cha Meza Huru kilichoruka ‘live’ kuanzia saa 9 mchana.

Akiwa mgeni mwalikwa sambamba na Afisa Sanaa wa Basata, Bi Bona Masenge, Nikki akapata wasaa wa kutoa ya moyoni juu ya mada iliyowekwa mezani iliyopewa jina la “Wasanii na Maadili”.

Wakati Bi Bona Masenge akionyesha namna wasanii wanavyotakiwa kubeba dhima ya kulinda maadili, Nikki wa Pili akaonyesha jinsi ambavyo wasanii wanajengwa (aidha kwa makusudi au bahati mbaya) kwenda kinyume na maadili.

Nikki akasema ifike wakati tujiulize hawa wasanii wanatoka wapi? Kwenye familia zipi? Je familia wanazotoka zina maadili? Jamii iliyowazunguka ina maadili? Kazi zao ambazo hazina maadili zinapokewaje na mashabiki wao?.

Msanii huyo akafafanua kuwa maadili ni jambo pana na haliishii kwenye sanaa tu bali hata kutoa na kupokea rushwa ni kinyume na maadili, kutoa habari ya kupotosha jamii ni kinyume cha maadili, kuchochea vita ni uvunjifu wa maadili.

Nikki wa Pili akasema kufungia nyimbo za Kitanzania kurushwa kwenye TV kwasababu hazina maadili, lakini wakati huo huo nyimbo za nje zenye maadili mabovu zikiendelea kurushwa kwenye vituo vya televisheni vya nyumbani, ni kichocheo cha uvunjifu wa maadili.

Katika kipindi hicho kilichoongozwa na watangazaji Hawa Hassan na Sam Mahela, Nikki akasema ifike wakati kuwe na upendeleo kwa wasanii wenye maadili ili kuwavutia wasanii wote kufuata njia hiyo.

“Kama msanii asiye na maadili hatengwi na taasisi za sanaa wala vyombo vya habari, basi tutegemee kuwaona wasanii wavunjifu wa maadili wanaendelea kuchanua,” alisema Nikki.
 Kutoka kushoto ni mtangazaji Hawa Hassan, Nikki wa Pili, mtangazaji Sam Mahela na Bi Bona Masinge wa Basata kabla kuunza kuumana kwa hoja
Hawa Hassan, Nikki wa Pili, Sam Mahela na Bi Bona Masinge wakiwa kwenye Meza Huru

No comments