OMOG AGOMA KUZUNGUMZIA HATMA YA SIMBA KWENYE MBIO ZA UBINGWA WA LIGI KUU

KOCHA wa Simba, Joseph Omog amesema kwa sasa hataki kuzungumzia ubingwa wa Ligi Kuu kutokana na changamoto zilizoko mbele yake.

Omog amesema, Simba inakumbana na vikwazo vikubwa kuwania taji hilo na changamoto ya kwanza wanayokabiliana nayo ni kutoka kwa timu pinzani zilizoko kwenye hatari ya kushuka daraja, zinazopigania kubakia Ligi Kuu.

Amesema, timu hizo zinaonyesha upinzani mkubwa katika mechi ambazo wanaenda kukutana nazo, hali inayompa hofu ya kutwaa taji hilo.

Aliongeza kuwa, kingine kinachompa hofu ya ubingwa ni presha ya wachezaji na viongozi kwenye timu katika kuwa na kiu ya ubingwa, hali inayosababisha wawe wanaingia uwanjani na woga wanapocheza mechi na kusababisha wachezaji kucheza kwa kutojiamini.

“Kiukweli ni mapema sana kuzungumzia ubingwa wa Ligi Kuu kutokana na changamoto kadhaa tunazopitia ambazo huenda zikakwamisha ndoto zetu.”

“Kama unavyojua, zipo baadhi ya timu ambazo ziko kwenye hatari ya kushuka daraja zinazopambania kubaki Ligi Kuu, ndizo zinazotupa changamoto ya ubingwa.”

“Kingine ni presha ya ubingwa iliyopo katika timu yetu, inayofanya wachezani na viongozi kuingia uwanjani na hofu ya kupoteza mchezo,” alisema Omog.

Hata hivyo, kocha huyo amesema nia yake ni kuhakikisha kuwa wanatwaa kila taji ambalo liko mbele yao, ili kuiandikia Simba historia mpya.


“Siku zote nataka mafanikio ila mambo yanayotokea kinyume cha matakwa yangu ndio yananichanganya,” alisema.

No comments