PICHA 20: NANI ZAIDI YA TAARAB YAACHA GUMZO TRAVERTINE …Khadija Yussuf, Mwasiti, Mcharuko watoana jasho


Hili ni moja ya maonyesho bora kabisa ya taarab kutokea ndani ya mwaka huu - waimbaji watano wa taarab na bendi zao tano wamefanya onyesho la kihistoria ndani ya ukumbi wa Travertine, Magomeni jijini Dar es Salaam.

Licha ya mvua kukatisha onyesho hilo kwa takriban saa nzima kuanzia saa 6 hadi 7 usiku, lakini burudani iliyopatikana ukumbini hapo ilikuwa si ya kitoto.

Saluti5 ilishuhudia ukumbi ukiwa umefurika mamia ya mashabiki wa taarab na pengine kama si mvua kunyesha, basi Travertine pangekuwa hakuna pa kuweka mguu.

Mwamvita Shaibu wa Ogopa Kopa akiwa na wimbo wake “Kunguni wa Mwendo Kasi”, Mwasiti Kitoronto wa Jahazi na wimbo wake “Nataka Jibu”, Khadija Yussuf wa Wakali Wao kupitia wimbo “Sina Uzuri wa Sifa”, Fatma Mcharuko wa Yah TMK na kitu “Siwaguni Siwakohoi” pamoja na Hanifa Maulid Jike la Chui na wimbo “Ishu Pambe” akisindikizwa na Funga Kazi Modern Taarab, walishindanishwa ili kupata nani mkali zaidi ya mwenzie.

Lakini kabla ya mpambano wao, ilitangulia burudani ndefu kutoka kwa Utalii Excellent Modern Taarab, kisha akafuata malikia wa mipasho Khadija Kopa aliyeuteka ukumbi na wimbo “Mjini Chuo Kikuu” kabla mvua haijashuka na kuleta ‘likizo’ ya saa nzima.

Baada ya mvua kukatika ndipo mpambano ulipoanza, Mwamvita Shaibu akifungua pazia, akafuata Mwasiti Kitoronto kisha Khadija Yussuf halafu Fatma Mcharuko kabla Hanifa Maulid hajafunga pazia.

Licha ya waimbaji hao watano kuchuana vikali, lakini ukweli usio na chenga ni Mwasiti Kitoronto, Khadija Yussuf na Fatma Mcharuko ndiyo waliokuwa ‘roho’ ya mpambano huo kwa namna nyimbo zao zilivyochuana jukwaani na kupokelewa kwa shangwe nyingi.

Khadija Yussuf ilikuwa ni kama hana mpinzani kwa upande wa uimbaji akitumia sauti yake tamu ambayo kuiiga yataka uache kazi na kufanya kazi.

Mwasiti Kitoronto hakushikika kwa meseji yenye michomo mikali iliyowafanya mashabiki wapagawe na waimbe nae mwanzo mwisho.

Fatma Mcharuko hakuwa na mpinzani kwenye kulimiliki jukwaa ambapo alionyesha uwezo wa kuimba huku akicheza kwa ufundi wa hali ya juu.

Lakini pia kimahesabu Mcharuko ndiye aliyetunzwa pesa nyingi na mashabiki, ndiye aliyetunzwa na wasanii wengi wa bendi pinzani, ndiye aliyewapa mzuka mashabiki wengi kupanda jukwaani kiasi cha kutishia usalama.

Yote kwa yote pambano lilikuwa tamu, Mwamvita Shaibu alionyesha kuwa kwenye wakali wa taarab na yeye yumo, Hanifa Maulid akadhihirisha kuwa wimbo wake wa “Ishu Pambe” ni gumzo la jiji.


Pata picha 20 za onyesho hilo ambalo lilinogeshwa sana na MC Dr Kumbuka kutoka Times FM.
 Khadija Kopa akishambulia jukwaa na wasanii wake
 Mvua iliposababisha 'likizo' ya saa nzima
 Dr Kumbuka MC wa onyesho 
Mwamvita Shaibu wa Ogopa Kopa

Waimbaji wa Ogopa Kopa
 Mwasiti Kitoronto wa Jahazi
 Waimbaji wa Jahazi
 Nyomi lililofurika Travertine
 Khadija Yussuf wa Wakali Wao
 Khadija Yussuf akitunzwa na mwanaye

Waimbaji wa Wakali Wao
 Fatma Mcharuko wa Yah TMK
 Mcharuko akimpa raha Mishi wa Jahazi
 Mcharuko akitunzwa na Khadija Yussuf
 Waimbaji wa Yah TMK
 Hivi ndiyo mashabiki walivyojitokeza kushuhudia mpambano wa waimbaji watano wa taarab
 Hanifa Jike la Chuki akiimba "Ishu Pambe"
 Waimbaji waliotikia kwa Hanifa Maulid
Hakika onyesho lilifana sana
Waimbaji wa Ogopa Kopa Naima Mohamed (kushoto) na Zena Mohamed wakifuatilia mpambano kwa makini


No comments