POINTI TATU ZA KAGERA SUGAR ZAZUA KIZAAZAA SIMBA SC... wanachama waanza kuwapigia kelele viongozi wao za "ondokeni"

KUPOKONYWA kwa Simba kwa pointi 3 na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, kumeanza kuleta joto baya kwa uongozi wa timu hiyo baada ya wanachama kuanza kuukataa uongozi wao.

Hatua hiyo inakuja kufuatia maamuzi ya Kamati hiyo inayoongozwa na wakili Richard Sinamtwa iliyotoa hukumu ya kuirudishia Kagera pointi tatu kufuatia ushindi wao wa uwanjani wa mabao 2-1.

Baadhi ya wanachama wa timu hiyo wameanza kuupigia kelele viongozi wao wakiwataka mara baada ya muda wao kumalizika wanapaswa kuachia ngazi kutokana na uzembe wa kukosa sh 300,000 za ada ya kukatia rufaa dhidi ya beki Mohamed Fakhi.

Wanachama hao walienda mbali zaidi wakisema Simba sio klabu yenye hadhi ya kugombea pointi za mezani tena dhidi ya Kagera Sugar hatua ambayo inaonyesha dhahiri kwamba uongozi wao umeshindwa kupigania ubingwa uwanjani.

“Unajua uongozi wetu umeshindwa kazi hili liko wazi, hivi kweli hawa watu wote wanajifanya wana hela wanashindwa kutoa laki tatu kulipia rufaa hii, ni aibu kubwa watuachie timu yetu tumewachoka,” alisema mwanachama mmoja.

“Simba sio timu ya kugombania pointi za mezani hasa na timu kama Kagera, hii ni dalili kwamba wenzetu kazi imewashinda, muda wao ikimalizika watuachie timu."

No comments