RAGE KUONGOZA MAPAMBANO YA KUDAI HAKI YA POINTI TATU ZA SIMBA FIFA

MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Alhaji Ismahil Aden Rage ndiye ambaye atabeba malalamiko ya klabu hiyo na kuyapeleka kwenye Shirikisho la Soka la kimataifa (FIFA), imefahamika.

Saluti5 inajua kwamba Rage ambaye ni bingwa wa kutafsiri kanuni za sheria za mchezo huu hapa nchini ameteuliwa rasmi kuiwakilisha Simba katika malalamiko mbalimbali.

Simba inadai kurejeshewa pointi zake tatu ambazo ilipewa na bodi ya Ligi baada ya Kagera Sugar kumchezesha beki Mohammed Fakhi ambaye alikuwa na kadi tatu za njano kabla ya mechi hiyo iliyochezwa mwanzoni mwa mwezi uliopita kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Lakini katika hatua iliyojaa utata mkubwa, Shirikisho la soka nchini (TFF) kupitia Kamati yake ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ikairejeshea Kagera pointi hizo tatu ikisema kwamba Simba imekata rufaa nje ya muda na haikulipa ada ya sh. laki tatu.

Hata hivyo sheria za FIFA zinasema kwamba kosa la mchezaji kucheza mechi akiwa na kadi tatu halina uhusiano na kukatiwa lufaa au kulipa ada bali ni kosa la moja kwa moja ambalo timu husika hupoteza  pointi tatu na mabao matatu.

Kamati ya masaa 72 iliyoipa Simba pointi tatu na ile ya Sheria na Hadhi iliyowapora Simba pointi hizo zote inakiri kwamba Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano na hapo ndipo Simba inaposhikilia na kuamua kwenda FIFA.

Rage mwenyewe juzi amesema yuko tayari kwenda FIFA kwa sababu Simba ni klabu yake na kuisaidia kupatikana kwa haki ni wajibu wake.

“Simba ni klabu yangu nikitumwa nitaifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa,” amesema Rage.

Lakini wakati Simba ikikusudia kwenda FIFA habari zinasema kwamba Shirikisho la soka nchini bado lenyewe linatafakari namna ya kuandika barua ya kuipora Simba pointi zake hizo tatu.

Chanzo kimoja kinasema kwamba TFF imekuwa ikigwaya namna ya kuandika barua hiyo na baadhi ya wakubwa katika Shirikisho hilo wameanza kulaumiana kwamba uamuzi wa kuipora Simba pointi zake unaeweza kusababisha matatizo makubwa kwa TFF.

“Sisi tulisema wazi kwenye kikao kwamba uamuzi huu wa kuipora Simba pointi ambazo tumewapa wenyewe kisheria unaweza kuleta matatizo makubwa kwa mpira wa Tanzania. 
Sasa watu hawataki kuandika barua, wanaona kama wanajikaanga wenyewe."

"Lakini hakuna jinsi nyingine, Simba lazima wapewe barua yao,” amesema mmoja wa viongozi wa Kamati mojawapo ya TFF.


Rais wa Simba, Evan Aveva amesema katika kikao na waandishi wa habari mapema wiki hii kwamba simba inakwenda FIFA kudai haki yake kwa sababu inajua kwamba uamuzi wa kuipora pointi tatu ambazo umefanywa na TFF haukuwa sahihi.

No comments