RAHMA MACHUPA: NIPO FUNGA KAZI LAKINI BADO NINA MKATABA WAKALI WAO

Mwimbaji anayeinukia kwenye taarab, Rahma Machupa amekiri kuwa ni kweli amejiunga na Funga Kazi Modern Taarab kwa ajili ya kuandaa wimbo wake mpya lakini akaweka wazi kuwa bado ana mkataba na Wakali Wao Modern Taarab.

Akiongea na Saluti5 kwa njia ya simu, Rahma alisema hadi sasa bado hajasema lolote kuhusu hatma yake ndani ya Wakali Wao na bado anajihesabu kuwa ni msanii wa kundi hilo kwa kuwa mkataba wake haujaisha, ingawa alisema lolote linaweza kutokea.

Rahma akasema amerekodi wimbo mpya na Funga Kazi Modern Taarab unaoitwa “Liwalo na Liwe” na muda wowote utaanza kusikika hewani.

“Watanzania wanataka kunisikia, Wakali Wao wameshindwa kunipa nyimbo, hivyo nimeona nitumie njia nyingine,” alisema Rahma Machupa na kuongeza kuwa mashairi ya wimbo huo yaliandaliwa siku nyingi na Captain Temba kabla hata hajajiunga na Wakali Wao.


“Tutakaa chini na kupitia mkataba wangu Wakali Wao na kuona kama vipengele vyote vinatimizwa, lakini kwasasa sina wa kumhofia juu ya kuachia wimbo wangu mpya na Funga Kazi. Kwa hili simuogopi kiongozi yoyote wa Wakali Wao,” alifunguka Rahma aliyejiunga na Walali Wao akitokea Jahazi Modern Taarab.

No comments