RAMADHANI MLUGURU AACHIA KITU CHA "KARIBU UKARIBIE"

YULE mkali anayetesa kwenye anga za mchiriku wa kisasa Bongo, Ramadhani Mluguru ameingia Studio za 442 Records zilizo chini ya mtayarishaji Mubanga na kuachia kibao kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Karibu Ukaribie’.

Mluguru ameongea na saluti5 na kusema kuwa kibao hicho kimebeba ujumbe mnono juu ya mtu anayemkaribisha mpenzi wake kwao huku akimtahadharisha juu ya hali halisi ya nduguze na vurugu zao.

“Watu wengi tumekuwa tukificha mapungufu ya familia zetu kwa wapenzi na hatimae kujikuta tukisababisha mitafaruku pale wapenzi hao wanapokuja kugundua wenyewe wakiwa tayari wameshaingia ndani,” amesema msanii huyo.

“Nimeamua kutunga wimbo huu ili kuikumbusha jamii kuona kwamba ni vyema kumueleza mpenzi wako kila kitu kuhusu ndugu zako ili hata akija kukutana na vituko vyao hapo baadae awe hana ugeni navyo tena,” ameongeza.


Amesema kuwa kibao hicho anachoamini kitawashika vilivyo mashabiki wa mchiriku, anatarajia kukiachia mapema wiki ijayo baada ya kukamilika kwa shughuli ya uchanganyaji Studio.

No comments