RAMADHANI SINGANO ASEMA HAJUTII KUIACHA SIMBA NA KUJIUNGA AZAM FC

BAADHI ya mashabiki wa Simba wanaamini kwamba kiungo wa zamani, Ramadhani Singano “Messi” anajuta kujiunga na Azam FC, klabu ambayo hajang’ara nayo sana kama alivyokuwa wakati yuko Simba.

Hata hivyo, Singano mwenyewe amesema kwamba hajutii kufanya hivyo ingawa amesema kwamba ameitakia kila la kheri Simba katika mechi yake ya mwisho na Mbao FC.

Akihojiwa na mtndao mmoja, Singano amesema hana sababu ya kuonea wivu mafanikio ya timu yake ya zamani inayoyapata msimu huu katika Ligi Kuu Tanzania bara.

Singano amesema ana furaha kucheza Azam akiwa na matumaini ya kupata mafanikio katika medani ya soka.

Simba imetinga fainali ya Kombe la FC na inatarajiwa kucheza na Mbao FC ya Mwanza katika mchezo utakaopigwa Mei 28, mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Singano amesema kwamba anajivunia kuchezea Azam kwakuwa ni klabu bora nchini licha ya kushindwa kupata mafanikio msimu huu.

“Najivunia kuwa mchezaji wa Azam, Napata kila ninachohitaji kwa wakati, kufanya vibaya msimu huu ni jambo la kawaida, hata klabu kubwa Ulaya huwa zinateleza,” amesema Singano.

Mchezaji huyo wa zamani wa Simba amesema ubora wa Azam katika nyanja mbalimbali unawashawishi wachezaji wengi kutamani kuitumikia klabu hiyo yenye maskani yake Chamazi,jijini Dar es Salaam.

Kumekuwa na habari kwamba Simba inataka kuwarejesha wachezaji wake wawili ambao wamejiunga na Azam na kwamba wanaotajwa kwenye dili hili ni Singano na Shomary kapombe.


Hata hivyo, kumedaiwa kuwa na mvutano katika Kamati ya usajili ya Simba kuhusu wachezaji ho wawili ingawaje Kapombe anaweza kurejea Simba kwasababu mkataba wake unatajwa kuwa unamalizika.

No comments