SAMATTA ASHEREHEKEA MECHI YA 54 KRC GENK

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samata juzi alikuwa kwenye furaha baada ya kutimiza mechi 54 tangu ajiunge na timu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji.

Samatta alicheza dakika zote 90 katika mchezo wao dhidi ya AS Eupen kwenye uwanja wa Kehrweg jijini Eupen ambapo walittoka sare ya mabao 1-1 akiwa amefunga jumla ya mabao 18.

Alianza kwa kusuasua msimu wake wa kwanza kutokana na ushindani wa namba ambao alikutana nao lakini hivi sasa amejihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza akicheza mfululizo na mchezo wake wa juzi ulikuwa wa 54 barani Ulaya.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ndiye Mtanzania pekee aliyeweka rekodi ya kucheza kwenye michuano ya Kombe la Europa kabla ya kutolewa na Celta Vigo ya Hispania kwenye hatua ya nane bora.


Samatta alitua Genk Baada ya kufanya vizuri kwenye klabu ya TP Mazembe ya nchini Congo DRC ambnapo alifanikiwa kubeba tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.

No comments