SHANIA WA BONGOFLEVA AINGIA STUDIO KUPAKUA KITU CHA “SHIRAWADU”

STAA mpya wa kike wa bongofleva anayekuja juu kwa kasi hivi sasa, Shania Kabeya leo ameingia Studio za "442 Records" zilizo chini ya mtayarishaji Mubenga kurekodi kazi yake mpya inayokwenda kwa jina la "Shilawadu."

Hiyo ni baada ya wiki iliyopita mwanadada huyo mfanyabiashara maarufu wa vipodozi, kupakua kazi yake ya kwanza inayokwenda kwa jina la "Penda Unapopendwa" iliyoko kwenye miondoko ya mchiriku wa kisasa.

Shania ameitonya saluti5 kuwa, "Shilawadu" ni kibao kilichoko kwenye miondoko ya mduara ambacho mashabiki watashuhudia akiimba kwa mabadiliko makubwa kutoka kwenye mchiriku aliorekodi awali kwenye wimbo "Penda Unapopendwa."

“Nimeamua sasa kuja na mduara ili kuwadhihirishia mashabiki wa muziki kuwa nina uwezo wa kuimba katika miondoko yoyote na nikapasua,” amesema Shania ambaye kiuimbaji na kimuonekano anashabihiana na msanii Shaa.

Akielezea sababu ya kuingia Studio haraka baada ya kuachia kibao chake cha kwanza, Shania amesema nia yake ni kuwa na vibao vingi vitakavyomtambulisha kwa wepesi mbele ya mashabiki na kwamba ataachia kazi mpya kila atakaporekodi.

No comments